June 09, 2019

BALOZI SEIF ALI IDDI AKAGUA MIRADI YA MAJI

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} Nd, Mussa Ramadhan akimpatia maelezo Balozi Seif  hatua zinazochukuliuwa na Mamlaka hiyo katika kuona Mradi wa ujenzi wa Tangi la Maji unazingatia Vigezo vyote.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifanya ziara ya kukagua eneo linalotarajiwa kujengwa Tangi kubwa na la Kisasa la Maji safi na salama la ujezo wa Lita Laki 1.5 katika Kijiji cha Kitope ndani ya Jimbo la Kiwengwa.
Balozi Seif akiupongeza Uongozi wa Jimbo la Kiwengwa kwa jitihada unazochukuwa za katika usimamizi wa kuondosha changamoto zinazowakabili Wananchi wao. Picha na – OMPR – ZNZ.

Unguja, Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameziomba na kuzikumbusha Taasisi na Makampuni yanayojitolea kusaidia huduma za Kijamii nchini kuzingatia mahitaji halisi ya Wananchi ili misaada pamoja na Miradi wanayoigharimia iweze kukidhi vigezo sahihi.
Alisema ipo miradi kadhaa ya wananchi akatolea mfano huduma za maji safi na salama inayopata nguvu za Uwezeshaji moja kwa moja kutoka kwa Taasisi Wahisani inapaswa kwenda sambamba na ukuaji wa maeneo hasa Miji Midogo iliyopo Wilayani na Mikoani inayotokana na ongezeko la Idadi ya Wakaazi wake.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo alipofanya ziara fupi ya kukagua eneo linalotarajiwa kujengwa Tangi Jipya na la Kisasa katika Mtaa wa Kitope baada ya lile liliopo kuachakaa na kushindwa kukidhi mahitaji halisi ya sasa kutokana na kuongezeka kwa Idadi ya Watu.
Ziara hiyo pia ilikwenda sambamba na kukagua ujenzi wa Mnara utakaokuwa na uwezo wa kuhifadhi Maji katika Matangi Mawili yenye ujazo wa Lita  Elfu kumi kila Moja katika Kijiji cha Kitope Muembe Majogoo ndani ya Jimbo la Kiwengwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema umuhimu wa Huduma za Maji safi na Salama unaeleweka na kila Mwana Jamii suala ambalo ipo haja kwa washirika wenye uwezo na Taaluma kulitia maanani jambo hilo katika kuona changamoto zinazowakabili Wananchi katika kupata huduma hiyo linaondoka.
Balozi Seif  aliwapongeza Viongozi kuanzia Wadi hadi Jimbo la Kiwengwa kwa jitihada wanazoendelea kuzichukuwa katika kusimamia mapambano dhidi ya changamoto mbali mbali zinazowakabili Wananchi wao.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Nd. Mussa Ramadhan alisema upo mpango wa hivi karibuni wenye muelekeo wa kujenga Tangi jengine jipya la kuhifadhia Maji safi na salama katika eneo la Kitope.
Nd. Mussa alisema ujenzi wa Tangi hilo litakalokuwa na ujazo wa lita Laki Moja na Nusu chini ya ufadhili wa Washirika wa Maendeleo umekuja kufuatia lile la asili kuchakaa pamoja na ujazo mdogo wa Lita 50,000 ambapo kwa sasa mahitaji ya huduma hiyo yameongezeka kutokana na kukua kwa Vitongoji.
Alisema Mamlaka ya Maji Zanzibar ikiwa msimamizi na mshauri muelekezi wa Ujenzi wa Mradi huo wa Tangi la Maji tayari imeshatoa michoro na harakati za kumpata mjenzi wa Tangi hilo ndani ya kipindi cha Miezi Miwili kuanzia sasa umeanza.
Naye Diwani wa Wadi wa Mbaleni Ndugu Hassan Ameir Abdulla  alisema Ujenzi wa Mnara wa kuhifadhia Matangi ya Maji Mawili yenye Ujazo wa Lita Elfu Kumi Kila Moja uko katika hatua nzuri kwa lengo la kuwaondoshea tatizo la Huduma hiyo inayowasumbua kwa muda mrefu sasa.
Nd. Hassan alimueleza Balozi Seif kwamba Mradi huo unaokisiwa kugharimu zaidi ya shilingi Milioni 35,000,000/- za Kitanzania unatarajiwa kukamilika rasmi kabla ya Mwezi wa Nane Mwaka huu.
Diwani huyo wa Wadi wa Mbaleni aliahidi kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar aliyekuwepo kwenye ziara hiyo kwamba Timu yao itakuwa tayari kushirikiana na Wahandisi wa Mamlaka ya Maji katika kuona Mradi huo unafanikiwa vyema katika kiwango kinachokubalika Kitaalamu.
 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
09/06/2019.

No comments:

Post a Comment

Pages