June 09, 2019

RED CROSS YAWAKUMBUKA WAATHIRIKA WA MAFURIKO KIGOGO, TANDALE


Wafanyakazi wa Red Cross wakitoa misaada ya kibinadamu kwa watu waliokumbwa na mafuriko katika Kata za Kigogo na Tandale jijini Dar es Salaam.

 
 
Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross) kimetoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 200 kwa kaya 500 zilizopo kata ya Kigogo na Tandale jijini Dar es Saalam.

Msaada huo umetolewa katika kaya hizo zenye watu 2000 kufuatia kukumbwa na mafurukio yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha Mwezi Mei mwaka huu na kuleta maafa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhi msaada huo Meneja wa Kujiandaa kukabiliana na maafa kutoka Red Cross, Jonston Weston alisema msaada huo uliyotolewa ni magodoro, ndoo na madumu ya maji, Vyombo vya jikoni, sabuni, blanketi za kujifunika, vyandarua na vifaa vingine kwa ajili ya wanawake.

Alisema msaada huo umewalenga wananchi wale ambao nyumba zao ziliathiriwa vibaya na mafuriko na kuongeza kuwa vipo vigezo mbalimbali vilitumika kuwapata watu hao hivyo wanaamini kuwa kila mwananchi atapana na mambo yatakwenda kama walivyopanga.

"Hizi kaya ambazo wanapewa msaada huu ni sehemu ya zile zilizoathirika vibaya, kutokana na vigezo vyetu mbalimbali tulifanikiwa kuzipata kaya hizo, miongoni mwa watu waliopata msaada huo ni zile familia zenye walemavu na watoto wadogo.

Hata hivyo katika kila kaya tumetoa magodoro mawili, ndoo mbili na madumu ya maji, blanket mbili, sabuni miche minne, vifaa vya wanawake pamoja na seti moja ya vyombo vya jikoni, vitu vingine ambavyo tutavitoa kama muendelezo wa msaada wetu ni vipeperushi vinavyoelekeza namna ya kukaa katika mazingira safi ili kuepuka kupata magonjwa ya milipuko, " alisema.

Naye Meneja wa Kukabiliana na Maafa Red Cross, Vivaoliva Shoo alisema licha ya msaada huo pia wanampango wa kuwapatia fedha za kujikimu kaya hizo ili ziweze kujinunulia mahitaji mengine wanayoyaona yanawafaa.

"Mpango huu wa kutoa fedha hatujauanza bado tunataka kwanza kukaa na serikali ili tuweze kuangalia tutawezaje kufanikisha, hata hivyo msaada huu tuliyoutoa tunalengo la kuwapunguzia makali waliyoyapata wananchi hawa, " alisema.

Alisema wanamini msaada wa magodoro na blanketi utawasaidia wananchi hao hasa watoto kulala mahali pazuri na kujikinga na baridi wakati wa usiku pia ndoo na madumu ya maji yatawasaidia kuteka maji safi na kuyatumia kwa matumizi ya nyumbani.

Kwa upande wake Neema Nestory mkazi wa kigogo aliyepata msaada huo alisema anawashukuru Red Cross kwa kuwasaidia hivyo watahakikisha wanavitunza vitu hivyo na kuvitumia kwa matumizi yanayofaa.

"Tulipata mafurukio mimi binafsi nilipoteza kila kitu lakini letu nimefarijika na nimepata tumaini jipya ninauhakika nitalala mahali pazuri, nitajifunika lakini pia nitakula na kuchota maji ambayo nitayahifadhi mahali safi na salama, " alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages