June 07, 2019

NMB YATOA MSAADA WA MADAWATI 150 NA VIFAA TIBA WILAYANI MKURANGA

 Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mwandege wilayani Mkuranga wakibeba madawati na viti mara baada ya kukabidhiwa na viongozi wawakilishi wa Benki ya NMB.Benki ya NMB imezipiga jeki shule tatu za sekondari na kituo cha afya wilayani Mkuranga vifaa vyenye thamani ya milioni 20.
 Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikali wa NMB, Bi. Vicky Bishubo (aliyesimama) akiwasalimu wakazi wa Mkuranga kabla yakukabidhi  madawati 150 na viti vyake kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga,  Filberto Sanga (mwenye suti ya khaki) katika hafla ya makabidhiano yaliofanyika Sekondari ya Mwandege. Benki ya NMB imezipiga jeki shule tatu za sekondari na kituo cha afya vifaa vyenye thamani ya milioni 20.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga,  Filberto Sanga  akitoa neno la shukrani kwa NMB katika hafla ya makabidhiano yaliofanyika Sekondari ya Mwandege baada ya kupokea msaada wa madawati 150 na viti vyake.Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikali wa NMB, Bi. Vicky Bishubo.  Benki ya NMB imezipiga jeki shule tatu za sekondari na kituo cha afya vifaa vyenye thamani ya milioni 20.


Na Mwandishi Wetu, Mkuranga 

BENKI ya NMB imekabidhi msaada wa madawati 150 na meza zake kwa shule tatu za sekondari pamoja na vifaa tiba na vitendea kazi katika Kituo cha Afya cha Kisiju Wilaya ya Mkuranga vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 20.

Shule zilizonufaika na msaada huo wa madawati pamoja na meza zake 150 yote yakiwa na thamani ya shilingi milioni 15 ni Sekondari ya Mwandege, Vikindu na Kiimbwanindi zote za Wilaya ya Mkuranga.

Akikabidhi msaada huo leo Wilayani Mkuranga kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga,  Filberto Sanga, Mkuu wa Kitengo cha Biashara za Serikali wa NMB, Bi. Vicky Bishubo alisema kituo cha afya kimekabidhiwa vitanda vitano na magodoro, kitanda kimoja maalum cha kujifungulia na mashuka 53 ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuboresha huduma za afya.

Bi. Bishubo alisema thamani ya msaada wote yaani madawati na viti vyake 150 pamoja na vifaa tiba ni shilingi milioni 20 na Benki ya NMB itaendelea kuchangia huduma za kijamii maeneo mbalimbali kadri hali inavyoruhusu.

Aidha alisema licha ya benki yao kupokea maombi mengi ya msaada wa kijamii imekuwa ikitoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu, afya pamoja na misaada ya hali na mali yanapotokea majanga kwa wananchi.

"Ndugu mgenia rasmi kwa mwaka 2019, Benki ya NMB imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja (1) kwa ajili ya kuchangia maeneo ya jamii ikiwemo kusaidia sekta ya afya na elimu. Kiasi hiki kinatufanya kuwa benki ya kwanza katika kuchangia maendeleo kuliko benki yoyote nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bw. Sanga akipokea msaada huo aliishukuru Benki ya NMB kwa msaada wake kwani upendo waliouonesha kwa Wanamkuranga utaendelea kudumu na kuiendeleza wilaya hiyo kimaendeleo.

Alisema msaada wa madawati umenusuru idadi kubwa ya wanafunzi ambao awali walishindwa kuendelea na masomo kwa shule zao kukosa madawati lakini sasa zimefunguliwa baada ya kupokea msaada huo na wanafunzi wanaendelea na masomo.

"...Wilaya yetu ilikuwa na shule tatu ambazo zilikuwa na changamoto kubwa ya madawati baada ya kuzianzisha, lakini msaada huu wa madawati na viti 15o kwa kweli umetufaa na umekuja kwa wakati muafaka," alisema Mkuu huyo wa Wilaya ya Mkuranga.

No comments:

Post a Comment

Pages