June 08, 2019

SERIKALI YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUKUZA UTALII NCHINI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Mihayo wakipewa maelezo na Wily hida kuhusu uimara wa gari maalum ya kubeba watalii jinis inavyoweza kuhimili hali zote pindi ikiwa mbugani na watalii mara baadfa ya  kufungua Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019 jijini Arusha. (Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii).


    WMU – ARUSHA
 
Serikali imesema kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi waliowekeza katika Sekta ya Utalii na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili kwa lengo la kuimarisha sekta hiyo na kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu wakati akifungua Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019 jijini Arusha.

Amesema ushirikiano huo unalenga kuifanya sekta ya utalii iwe zao namba moja na chanzo kikuu cha mapato nchini na kuongeza kuwa Tanzania inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege kwa lengo la kufungua shughuli za utalii katika maeneo yote yenye vivutio vya utalii.

Mhe.Kanyasu amesema kufanyika kwa maonesho hayo ambayo ni makubwa mara mbili ya yale yaliyofanyika mwaka jana ni ishara ya kukua kwa sekta ya utalii na kueleza kuwa washiriki kutoka nchi 40 za ndani na nje Afrika na mashariki ya nje yameshiriki.

“Maonesho haya yana sura ya Kimataifa hili linatambulika kwa kuona washiriki hao sisi kama nchi tumepata bahati, tungeweza kutumia gharama kubwa kuwaleta hawa watoa huduma za utalii huko kwenye nchi zao, hawa wamekuja wenyewe na hii imesaidia kampuni za Tanzania badala ya kwenda nje kuuza biashara zao wamekutana na kampuni za kimataifa hapa hapa Tanzania” Amesema Mhe. Kanyasu.

Amesema onesho la KARIBU KILIFAIR linasaidia kukuza utalii nchini kutokana na umuhimu wake wa kuuza huduma na bidhaa za utalii kwa kutangaza fursa mbalimbali zilizopo hapa nchini na kuongeza kuwa ili utalii uweze kukua ni lazima kazi ya kutambulisha na kuuza bidhaa za utalii ifanyike.

Mhe. Kanyasu amezitaka taasisi za uhifadhi zilizo chini ya Wizara ambazo zinashiriki maonesho hayo zikiwemo TANAPA, Ngorongoro, TAWA, Bodi ya Utalii Tanzania na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) zifikiri kibiashara na kutafuta wawekezaji wapya watakaowekeza na kufanya biashara kwenye Mapori ya Akiba, Misitu ya Asili na hifadhi za Taifa ambazo bado hazijapata wawekezaji ili nazo zichangie katika pato la Taifa.

“Tunataka taasisi zote wakati zinashiriki uhifadhi zifikiri kibiashara, tunataka tuondokane na mfumo wa kizamani wa kufikiri kuhifadhi bila kufikiri kibiashara, tuna mapori mengi ambayo ambayo hayaingizi fedha, tunataka taasisi za usimamizi wa mapori haya watafute wawekezaji kwa kuainisha fursa za uwekezaji zilizopo” Amesisitiza Mhe. Kanyasu.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya ukanda wa kusini ikiwemo barabara, ununuzi wa ndege kubwa za kisasa na kuboresha viwanja vya ndege ili kufungua Utalii wa ukanda wa Kusini na kuongeza shughuli za utalii katika hifadhi za ukanda huo zikiwemo Ruaha Selous, Mikumi na Udzungwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Mihayo akizungumzia maonesho hayo amesema kuwa mwaka huu Tanzania imepata wageni wengi walioshiriki maonesho hayo kutoka ndani na nje ya Afrika.

Amesema ujio wa washiriki hao utasaidia kwa kiwango kikubwa kuitangaza Tanzania kimataifa na kusaidia kukuza na kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambaye na Mbuge wa Iringa mjini, Mhe. Peter Msigwa ameeleza kuwa ushiriki wa makampuni mengi ya utalii ya ndani na nje ya Tanzania unaeleta chachu katika dhana nzima ya kukuza utalii nchini.

“Hili ni jambo jema na lenye heri ambalo kwa kufanya maonesho haya yanasababisha tujulikane, biashara ni matangazo tunapokuwa tunajulikana ndani ya nchi na kimataifa inasaidia sana kukuza utalii” Amesema Mhe. Msigwa.

Mhe. Msigwa amesema ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali ni muhimu katika kukuza utalii nchini akibainisha kuwa hilo litaiwezesha serikali kuendelea kukusanya kodi kutoka sekta binafsi kwa lengo la kuendesha nchi.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya KILIFAIR ambao ni waandaaji wa maonesho hayo ya Kimataifa ya Utalii ya KARIBU KILIFAIR 2019, Bw.Dominick Shoo ameeleza kuwa maonesho hayo kwa mwaka huu yamewahusisha washiriki zaidi ya 450 kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Bw. Shoo ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa kwa sekta binafsi na kazi kubwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika ya kufungua vituo vipya vya utalii katika mikoa ya Kanda ya ziwa na kueleza kuwa wao kama wadau wa sekta binafsi wataendelea kuvitangaza vivutio hivyo kwa nguvu kubwa.

“ Ninaishukuru Serikali kwa kuweka msukumo mkubwa katika uanzishaji wa vituo vipya vya utalii na kazi kubwa inayoendelea ya kuboresha miundombinu, ninaamini utalii wa Tanzania utakua kwa kasi na hii inaashiria kwamba ushirikiano tunaoupata kutoka Serikalini utalii utakua kwa kasi kubwa na tutapata watalii wengi zaidi” Amesisitiza Bw. Dominick.

No comments:

Post a Comment

Pages