July 27, 2019

Bashungwa ataka ushirikiano kukuza soko la bidhaa SADC, EAC

Na Suleiman Msuya

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amewataka wamiliki wa viwanda  washirikiane na Serikali ili kuhakikisha soko la bidhaa zao linakuwa kubwa kwenye nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Bashungwa alisema hayo jana alipokutana na wafanyabishara na wamiliki wa viwanda wa Tanzania wakati wakielekea Wiki ya Viwanda ya SADC inayotarajiwa kuanza Agosti 5 hadi 9/2019 jijini Dar es Salaam.

Alisema Serikali imejipanga kushirikiana wamiliki wa viwanda pale ambapo itahitajika kufanya hivyo ili kujenga uchumi wa viwanda.

Alisema wazalishaji wanatekeleza asilimia 30 ya kuwepo kwa kiwanda hivyo Serikali inapaswa kusaidia asilimia 70 iliyobakia inatimia.

Waziri alisema masoko, mazingira sahihi na mikakati mingine inapaswa kufanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau.

Alisewataka wamiliki wa viwanda kutumia wiki hiyo ya viwanda ya SADC kama fursa pekee kuthibitishia umma wa nchi wanachama uwezo wa Tanzania katika uzalishaji.

"Ili sekta ya viwanda iwe na tija nchini nilazima wadau wote washiriki kwenye mikakati kwa kutumia uhusiano wa kikanda wa SADC na EAC," alisema.

Alisema alisema mkakati wake ni kuona viwanda vinavyozalisha kwa sasa vinatua changamoto zake ili viweze kukua na itasaidia kuhamasisha viwanda vipya.

 Alisema kasi hiyo ya kuimarisha viwanda inatakiwa kuendana na utekelezaji wa mkakati wa ufanyaji biashara huru (Blue Print).

"Iwapo soko la kanda hizo litatumika vizuri ni wazi matarajio ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania ya uchumi wa viwanda inatimia," alisema.

Aidha, Waziri Bashungwa alisema pamoja na mikakati mbalimbaki ya wizara yake pia wapo kwenye mapitio ya sheria na sera ya uendelezaji viwanda vidogo ili iendane na wakati husika.

Alisema mikakati yao ni kuona viwanda vya Tanzania vinakusa soko la ndani na nje ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Aliwataka wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara kutoa taarifa kuhusu vikwazo wanavyokutana navyo kwenye utekelezaji wa majuku yao.

Kwa upande wao wamiliki wa viwanda  waliomba Serikali kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zenye ubora duni kwa kuwa zinashusha soko la bidhaa za ndani.

Walisema viwanda vya Tanzania vinazalisha bidhaa bora na imara ila bidhaa hizo zinakutana na changamoto zikifika sokoni kwa kuwa bidhaa za nje zinauzwa bei ndogo.

"Mheshimiwa Waziri wiki ya viwanda ya SADC ni muhimu lakini tunaomba udhibiti uongezeke katika uingizaji wa bidhaa zisizo bora katika soko letu ni changamoto kubwa," walisema.

No comments:

Post a Comment

Pages