July 31, 2019

DK. BASHIRU AONYA WATAKAOPITIA MLANGO WA NYUMA KUWANIA JIMBO LA ILEMELA MWANZA

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dk. Bashiru Ally akizungumza na wana CCM katika mkutano Mkuu wa Jimbo la Ilemela tarehe 30 Julai 2019 kuelezea utekelezaji wa ilani ya Chama  cha Mapinduzi kama ilivyoahidiwa na Mbunge wa Jimbo hilo wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2015.
Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dkt Bashiru Ally amesema hatashangaa kuona mbunge wa jimbo la Ilemela ambaye ni Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu ujao 2020 kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake.
Dkt Bashiru alisema hayo tarehe 30 Julai 2019 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mkutano Mkuu wa Jimbo la Ilemela kuelezea utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoahidiwa na Mbunge wa Jimbo hilo wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2015.
Katibu Mkuu huyo wa Chama cha Mapinduzi alisema hakuna kumnadi tena Dkt Angeline Mabula kwa kuwa anazo sifa zinazomuwezesha kutetea kiti chake na yeyote anayetaka kuwania nafasi katika jimbo hilo ajue kiti hicho kishakaliwa pamoja na kata zake 19.
‘’Ole wake anayetaka kupita mlango wa nyuma, chama kina utulivu sitashangaa Dkt Mabula akipita bila kupingwa ‘’ alisema Dkt Bashiru.
Alionya Wabunge wa CCM waliozembea kufanya ziara za kutatua kero za wananchi  pamoja na kufanya vikao kwenye majimbo yao kuwa hawatakuwa na ulinzi wakati wa kinyanganyiro cha kupendekeza majina ya kuwania nafasi hizo na kusisitiza kuwa kipaumbele kitatolewa  kwa  wabunge waliokuwa wakichapa kazi.
Aliwaaambia wana Ilemela kuwa, kuna tofauti kubwa sana ya kimaendeleo wakati jimbo la Ilemela lilipokuwa chini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na sasa linavyoshikiliwa na Chama cha Mapinduzi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula alisema jimbo lake kwa sasa limepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta za elimu, Afya, Maji, Mindombinu, Uzalishaji na Mifugo, Viwanda na Biashara pamoja na Utamaduni na Michezo ukilinganisha na miaka iliyopita.
Akielezea maendeleo katika sekta ya Afya ndani ya jimbo hilo, Dkt Mabula alisema jimbo la Ilemela limefanikiwa kujenga zahanati mbili mpya alizozitaja kuwa ni Buganda na Lukobe, hospitali ya Wilaya pamoja na vituo vya afya vya Lumala na Nyamazogo.
Aidha, Mbunge huyo wa Ilemela alisema katika sekta ya elimu walifanikiwa kujenga shule mpya za sekondari za Kayenze, Angeline Mabula na Kisundi huku shule za msingi zikijengwa mbili za Kayenze ndogo pamoja na Ihalalo aliyoielezea kuwa ilijengwa kwa ushirikiano na serikali ya Korea kusini aliyoiita shule ya mfano na kubainisha kuwa wilaya ya Ilemela iliongoza kimkoa katika elimu huku ikishika nafasi ya sita katika kanda ya ziwa.
Akigeukia suala la migogoro ya ardhi katika jimbo lake ambapo yeye ni Naibu Waziri mwenye dhamana, alisema jimbo hilo lilikuwa na migogoro mikubwa ya ardhi kati ya wananchi na jeshi la polisi katika eneo la Kigoto, Jeshi la Wananchi na wakazi wa Nyagugulu na mgogoro uliohusisha wananchi wa Bwiru ambapo alieleza kuwa migogoro hiyo sasa imekwisha baada ya wananchi kupatiwa maeneo na wengine kulipwa fidia.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dkt Bashiru Ally ameonya dhidi ya wafanyabiashara wanaotumia lumbesa na vipimo visivyokubalika katika kupima mazao ya kilimo kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao na kuwataka wakuu wa mikoa, wilaya na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanasimamia suala hilo kwani utekelezaji wake umeonekana kusuasua.
Alisema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli alishatoa maagizo kwake na  Waziri Mkuu juu ya suala hilo na kubainisha kuwa watendaji wa serikali wanapaswa kulisimamia hilo na kusisistiza kuwa iwe Ushirika ama mtu binafsi matumizi ya vipimo visivyozingatia taratibu hayakubaliki na mtu wa kutoa taarifa ya matumizi yasiyofaa ya mizani ni wananchi kupitia CCM.

No comments:

Post a Comment

Pages