July 30, 2019

Kamati SADC yatakiwa kukamilisha maandalizi

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi, John Kijazi, akitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Joseph Bushweishaija na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Faraji Mnyepe (kushoto), baada ya kufanya ziara ya kuangalia maandalizi ya ukumbi wa Kimataifa Mwalimu Julius Nyerere (JNIC), utakaotumika kufanyia mkutano wa 39 SADC. (Picha na Suleiman Msuya).

Na Suleiman Msuya

KATIBU Mkuu Kiongozi, Mhandisi Balozi John Kijazi ameitaka Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuhakikisha maandalizi yanakamilika kwa asilimia 100 kabla ya mikutano kuanza Agosti 4/2019.
Aidha, Kijazi amewaomba Watanzania kutumia fursa ya mkutano wa SADC kufanyika nchini kuchochea uchumi wa Tanzania.
Katibu mkuu aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ukaguzi wa Ukumbi Julius Nyerere International (JNIC) utakaotumika kwenye mkutano huo kuanzia Agosti 4 hadi 18 mwaka huu.
Alisema amezunguka na kujinea ambapo maandalizi yanaenmdelea vizuri na kuitaka kamati kuongeza kasi ili kila kitu kikamilike ndani ya muda uliopangwa.
Balozi Kijaji alisema Tanzania inatakiwa kuonesha nchi wanachama wa SADC kuwa inaweza kufanya mambo makubwa hivyo maandalizi mazuri ni muhimu.
“Nimeona maandalizi yapo vizuri ila nitumie nafasi hii kuipa kamati ikamilishe kwa wakati kama ambavyo tumekubaliana,”alisema.
Alisema mkutano huo unatarajiwa kumkabidhiri Rais John Magufuli Uenyekiti wa SADC hivyo unapaswa kutumika vizuri ikiwemo maandalizi maziru ya mkutano huo.
Kijazi alisema mkutano huo utaanza Agosti 4 hadi 8/ 2019 kwa wiki ya viwanda ambapo zaidi ya washiriki 1,000 kutoka nchi wanachama wanatarajiwa kuonesha shughuli wanazofanya.
Pia alisema baada ya wiki ya viwanda kutakuwa na mikutano ya kitaalam, makatibu wakuu, mawaziri na Agosti 17 hadi 18/2019 utakuwa mkutano wa viongozi wakuu wa SADC.
Aidha, Balozi Kijazi amewaomba Watanzania kutumia mkutano huo kama fursa ya kiuchumi ili kuweza kuisukuma Tanzania katika uchumi wa viwanda.
Balozi alisema mkutano wa SADC utahitaji wafanyabiashara, wasafirishaji, wenye mahoteli, sekta ya utalii na nyinginezo hivyo Watanzania wanapaswa kuzichangamkia.
Katibu mkuu kiongozi aliwaasa waandishi wa habari nchini kutumia kalamu zao vizuri kwa kuandika mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ili nchi za SADC ziweze kujifunza na kunufaika.
Alisema Tanzania ina historia ndefu kwa nchi za SADC hivyo ni wajibu wa waandishi wa habari kuandika mema ambayo yamefanywa ili kuendelea kuitangaza nchi.
Mkutano wa SADC utashirikisha nchi 16 ambazo ni Tanzania, Malawi, Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Shelisheli, Mauritius, Angola, Comoro, Madagascar, Botswana, Eswantin, Namibia na DRC ambapo zaidi ya washiriki 1,000 wanatarajiwa kushiriki.

No comments:

Post a Comment

Pages