July 16, 2019

Kilosa wajipanga kuendeleza USM

  Meneja Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Endelevu (TTCS) Charles Leonard akitoa mada kuhusu mradi huo kwa madiwani wa kata mbalimbali wa Halmashauri ya Kilosa mkoani Morogoro walioshiriki warsha ya siku moja mjini hapo.Picha na Suleiman Msuya.

 
Na Suleiman Msuya, Kilosa
 
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Kilosa, Hassan Mkopi amesema wamejipanga kuendeleza Usimamzi Shirikishi wa Misitu (USM), baada ya Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Endelevu Tanzania (TTCS), maarufu 'Mkaa Endelevu' kufikia mwisho Novemba 2019.

Mkopi alisema mradi wa Mkaa Endelevu umefanya mapinduzi ya kijamii, kiuchumi na maendeleo hivyo wao kama wawakilishi hawana budi kuuendeleza kwa kutenga bajeti.

"Sisi madiwani tunapaswa kuendeleza mradi huu wa TTCS na USM kwa vijiji vipya wakati wafadhili wanaondoka. Hakuna shaka kuwa mradi huu umechangia huduma za kijamii kama elimu, afya, maji, kilimo, mazingira na nyinginezo kuboreka," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema madiwani wanapaswa kutumia nafasi zao kwa kutunga sheria na sera ambazo zitasaidia uendelezaji wa USM vijijini.

Mshauri wa Maliasili Mkoa wa Morogoro, Nanjiva Nzunda alisema mradi huo umekuwa na matokeo chanya hivyo madiwani wanapaswa kuendeleza baada ya mradi kufikia mwisho.

Alisema wao kama Serikali na wasimamizi wa maliasili wameona faida za mradi hivyo ni jukumu la halmashauri husika kuendeleza.

Meneja Mradi wa TTCS, Charles Leonard alisema mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asili Tanzania (TaTEDO) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo Uswis (SDC), utafikia kikomo Novemba mwaka huu.

"Sisi tunaamini mradi huu una tija tunaomba tukiondoka muendeleze kwani faida ni kubwa kulilo hasara," alisema.

Alitolea mfano kuwa hadi sasa vijiji 20 ambavyo vipo kwenye mradi 18 vina mpango wa matumizi bora ya ardhi, vijiji 20 vina ofisi za vijiji zenye thamani ya shilingi bilioni 1.

Alisema vijiji 15 kati ya 20 vimeanza kuvuna mkaa na mbao ambavpo zaidi ya shilingi bilioni 2.2 zimekusanywa na kunufaisha vijiji, wananchi na halmashauri.

No comments:

Post a Comment

Pages