July 22, 2019

SERIKALI KUWAJENGEA UWEZO MAKANDARASI WADOGO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akifungua kongamano la uhamasishaji na uanzishwaji wa umoja wa makandarasi na vikundi vinavyotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi, ukarabati wa matengenezo ya barabara lililofanyika katika Chuo cha Teknolojia Stahiki ya Nguvu Kazi (ATTI) mkoani Mbeya.


Na Mwandishi Wetu

Serikali imesema itawajengea uwezo makandarasi wadogo wanaotumia teknolojia ya nguvukazi (Labor Based Technology) katika ujenzi na ukarabati wa matengenezo ya barabara, madaraja na majengo ili kuhakikisha kuwa wanapata fursa zaidi za kushiriki na kushindana katika kazi zilizotengwa mahsusi kwa ajili makandarasi hao.

Hayo yalibainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, kwenye kongamano la uhamasishaji na uanzishwaji wa umoja wa makandarasi na vikundi vinavyotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi, ukarabati wa matengenezo ya barabara uliofanyika mkoani Mbeya katika Chuo cha Teknolojia Stahiki ya Nguvu Kazi (ATTI) na kuhudhuriwa na wakandarasi wadogo wadogo
zaidi ya 150.

Arch. Mwakalinga, alisema kuwa Wizara kupitia taasisi zake zinazotekeleza miradi ya ujenzi itaendelea kutumia sheria na kanuni zilizowekwa ili kuhakikisha kazi zilizoainishwa kwenye miradi ya ujenzi ikiwemo ukarabati na matengenezo ya barabara, madaraja na majengo zinafanywa na makandarasi  hao. 


"Wizara imeteua timu ya wataalam kupitia nyaraka mbalimbali za miradi ya ujenzi ili kuhakikisha asilimia 30 ya fedha zinazolipwa kwenye mikataba mbalimbali ya ujenzi zinaelekezwa kwa makandarasi wanaotumia teknolojia ya nguvu kazi", alisema Mwakalinga. 

Aliongeza kuwa upitiaji utafanyika kwa haraka chini ya wataalam hao ambapo anaamini watafanya kazi hiyo vizuri ili kubainisha vigezo ambavyo makandarasi hao wamekuwa wakivilalamikia kila siku katika utekelezaji wa kazi zao ili
vifanyiwe kazi.


Aidha Arch. Mwakalinga, alibainisha kuwa Serikali inatambua makandarasi hao ni chachu kubwa katika kutatua tatizo la ajira kwa wananchi hususani maeneo ya vijijini kwani mara nyingi wakandarasi hao hutumia vifaa na vibarua
wanaopatikana katika eneo la mradi.  


" Mbali na kuongeza ajira na kuimarisha usafiri hususani maeneo ya vijijini, serikali inaelewa fika mnachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kwa kodi mnayolipa kupitia kazi mnazozifanya" alisisitiza Mwakalinga.

Alisema ni jukumu la wakandarasi hao kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na kuwa na sauti moja katika kufuatilia fursa mbalimbali na maslahi yao na kupata ufumbuzi wa pamoja wa changamoto zinazowakabili. 


Awali akimkaribisha Katibu Mkuu huyo Mkurugenzi wa Barabara, Mhandisi Rogatius Mativila, alisema madhumuni ya kikao kazi hicho ni kujadili kwa pamoja masuala muhimu katika Sekta ya Ujenzi ili kuendeleza na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Nguvukazi katika kutekeleza matengenezo ya barabara, madaraja na majengo bila kusahau sekta nyingine nchini. 


Akiongea kwa niaba ya makandarasi hao, Bi Aurelia Mtui, alitoa shukrani za dhati kwa Serikali kwani amekuwa kwenye taaluma hiyo kwa miaka 18 na kwa mara ya kwanza wamekutana na Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi kuzungumzia changamoto zao na kuomba maazimio waliyokubaliana katika kikao hicho yafanyiwe kazi. 


 Serikali ilianzisha mpango wa kuendeleza matumizi ya teknolojia ya Nguvukazi tangu mwaka 2004 na kulingana na takwimu zilizopo hadi kufikia mwezi Juni 2019 jumla ya Makandarasi 267 walikuwa wamesajiliwa na bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) katika madaraja ya kutumia teknolojia ya nguvukazi.

No comments:

Post a Comment

Pages