July 20, 2019

SIMIYU, ARUSHA WANG’ARA BAISKELI MAJIMAJI SELEBUKA

Bingwa wa mbio za baiskeli kwa afya za Tamasha la Majimaji Selebuka, Masunga Duba, kutoka mkoani Simiyu, akimaliza mbio hizo za kilomita 100, zilizofanyika mkoani Ruvuma. (Na Mpiga Picha Wetu).
Mkurugenzi-Mwenza wa Taasisi ya So-Mi, Prof. Julian Murchison kutoka Marekani, akimpongeza baada ya kumvisha medali, bingwa wa mbio za baiskeli kwa afya Tamasha la Majimaji Selebuka, Masunga Duba zilizofanyika jana Julai 20, mwaka huu mkoani Ruvuma.
Mshindi wa mbio za baiskeli kwa afya Tamasha la Majimaji Selebuka 2019, Masunga Duba kutoka mkoani Simiyu akikabidhiwa kitita chake cha milioni moja na Mkurugenzi Mwenza wa Taasisi ya So-Mi, Prof. Julian Murchison ambayo ndiyo waandaji wa tamasha hilo.
 Boniphace Masunga aliyeshika nafasi ya pili katika mashindano ya mbio za baiskeli kwa afya zilizoandaliwa na Tamasha la Majimaji Selebuka mjini Songea, Ruvuma akimaliza mbio hizo zilizofanyika jana Julai 20, mwaka huu.


 Na Mwandishi Wetu, Songea
MWENDESHA Baiskeli kutoka Simiyu, Masunga Duba, ameendeleza ubabe katika Tamasha la Majimaji Selebuka 2019 baada ya kutetea ushindi alioutwaa mwaka jana.
Katika mbio hizo za baiskeli kwa afya zilizoanzia Makumbusho ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji hadi eneo la Liganga kisha kurejea, ikiwa ni umbali wa Kilomita 100, Masunga alishinda akitumia saa 2:50.43 akiboresha muda alioutumia mwaka jana wa saa 2:53.05.
Nafasi ya pili pia ilikwenda mkoani Simiyu kwa Boniphace Masunga aliyetumia saa 2:51.01 huku nafasi ya tatu ikinyakuliwa na Denis Julias kutoka Arusha saa 3:15.00.
Masunga kwa ushindi huo alijinyakulia kitita cha Sh. Milioni 1 na medali ya dhahabu huku mshindi wa pili Boniphace akilamba Sh. 700,000 na medali ya fedha wakati mshindi wa tatu Denis akiondoka na Sh. 500,000 na medali ya shaba.
Mshindi wa nne aliibuka Ombeni Mbilinyi wa Iringa aliyetumia saa 3:15.03 na kuzawadiwa Sh. 300,000 na medali ya ushiriki huku nafasi ya tano ikienda kwa Asso Gadas kutoka Dar es Salaam saa 3:15.41 na kujipoza kwa Sh. 100,000 na medali ya ushiriki.
Ipyana Mbogela kutoka Iringa mshindi wa tatu mwaka jana, aliporomoka hadi nafasi ya sita akitumia saa 3:20.41, nafasi ya saba ikaenda kwa Kwilasa John wa Manyara saa 3:22.45, wa nane Hagai Sanga saa 3:30.53, Elias Tala alitumia saa 3:40.11 huku kumi bora ikifungwa na Abdul Kajenje aliyetumia saa 3:54.22 wote kutoka Mbeya.
Washindi wa sita hadi kumi kila mmoja alipata kifuta jasho cha Sh. 50,000 na medali za ushiriki.
Tukio hilo la Baiskeli, ndilo lilikuwa la kuhitimisha tamasha hilo ambalo lilikata utepe Julai 13 kwa mchezo wa Riadha kwenye Uwanja wa Majimaji mjini hapa.
Akizungumza wakati wa kufunga tamasha la mwaka huu, Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Songea Mississippi (So-Mi), ambao ndio waandaaji wa tamasha hilo, Prof. Julian Murchison, alisema lengo la kuanzishwa kwa tamasha hilo ni kuinua vipaji na fursa mbalimbali mkoani Ruvuma na ndio maana wamekuwa wakilifanya kila mwaka.
“Tamasha hili tuna malengo mbalimbali, tunataka kuinua vipaji hususan kwa vijana mkoani Ruvuma, kutoa fursa na pia kujenga mahusiano bora kati ya mji mkuu wa Ruvuma, Songea na Mississippi ninakotokea…Kupitia mahusiano haya tunabadilishana mawazo ya kujenga vitu mbalimbali baadaye,” alisema Prof. Julian.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tamasha hilo, Nathan Mpangala, alihuzunishwa na wenyeji kutojitokeza mwaka huu kwenye mchezo huo tofauti na misimu minne toka lianzishwe tamasha hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages