Mkuu wa Wilaya ya Songea, Poreleti Kamando, akipata maelezo kutoka kwa Mwakilishi wa Kikundi cha Jeam's Product wazalishaji wa Wine ya Jema, Judith Tarimo, wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Majimaji Selebuka 2019 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma juzi. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na Mwandishi Wetu
UMAARUFU wa tamasha la kila mwaka la Majimaji Selebuka
linalofanyika mjini Songea, Ruvuma umezidi kupaa mpaka nje ya mipaka ya
Tanzania huku idadi ya wageni ikiongezekana safari hii jukwaa la wajasiriamali
limevamiwa na mfanyabiashara Mkenya ambaye amekuwa gumzo kwa ubunifu wa bidhaa
zake.
Tamasha hilo la wiki nzima linaendelea kwenye Uwanja wa
Majimaji, Songea ambapo ni mwaka wa tano likiratibiwa na Taasisi ya
Songea-Mississippi (So-Mi).
Lucas Seguda, Mtanzania anayeishi Kenya anajishughulisha kufuma
kwa mkono vitu mbalimbali kama mazulia makubwa kwa madogo, makanyagio, mataulo
huku bidhaa zake zikiwa na nakshinakishi kama picha za wanyama na ujumbe
unaohamasisha vita dhidi ya ujangili.
“Sio suala la kufuma bidhaa, naangalia ni jinsi gani naweza
kuhimiza jamii kwa jambo lolote la maana, mfano kupinga mauaji ya Temba na
kutunza mazingira.
“Kazi hii niliianza mwaka 2012 na kweli nimepiga hatua kubwa
sana, soko langu kuu liko Kenya na ndipo nafanyia biashara zangu siku zote,
japo mimi ni Mtanzania wa Simiyu,” alisema Seguda na kuongeza.
“Nililazimika kuangalia mbali zaidi, hapa Tanzania hatuna
utamaduni wa kununua vitu vya asili kama hivi vya kufumwa, tunakimbilia vya
wazungu, lakini wao wanakimbilia vya kwetu. Huko Kenya wanapenda sana na zulia
kubwa huliuzwa mpaka dola 400 (zaidi ya laki tisa) ila kwetu pamoja na kuyauza
laki na nusu bado ni mtihani.”
Wananchi wamezidi kumiminika kwenye mabanda ya wajasirimali
wengi wakitaka semina ya ufumaji huo huku mabanda mengi zikipatikana huduma ya
dawati la jinsia na watoto, kufungua akaunti kwa benki za NMB na CRDB, Wizara
ya Utalii kwa Mbuga ya Taifa ya Ruaha, watengezaji mvinyo na bidhaa nyingine
nyingi.
No comments:
Post a Comment