WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza
Wizara ya Maliasili na Utalii isimamie uboreshaji wa eneo la mnara wa
Zinjathropus ili paweze kuvutia zaidi.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatatu,
Julai 22, 2019) wakati akizungumza na wananchi na viongozi waliohudhuria
maadhimisho ya miaka 60 ya kumbukizi ya ugunduzi wa fuvu la Zinjathropus Bosei, eneo la bonde la
Olduvai, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.
Maadhimisho hayo yamefanyika ndani ya
hifadhi ya Ngorongoro sambamba na uzinduzi wa makumbusho ya Dkt. Mary Leakey.
Mnara wa Zinjathropus na Homo habilis
umejengwa kwenye hifadhi ya Ngorongoro karibu na njia panda ya kuelekea bonde
la Olduvai.
"Kwenye mnara wa Zinjathropus na Homo habilis pasiachwe kama palivyo. Pajengwe seng'eng'e kuzunguka
eneo lile lakini pia paweke kibanda cha mlinzi ambaye pia atakuwa anatoa
taarifa kwa wageni wanaopita hapo.”
"Mtafute vijana kadhaa ambao ni
wenyeji wa eneo hili, wafundishwe historia kamili kisha wapewe ajira hizo.
Kibanda kikijengwa kwa juu kiwe na vioo ili anayelinda aweze kuona pande zote
na pia muweze kumkinga na vumbi na upepo mkali wa eneo lile."
Waziri Mkuu pia alitembelea korongo la
Frida Leakey, (mahali ambapo zinjathropous
aligunduliwa) na kupata maelezo juu ya kugunduliwa kwa fuvu la mtu wa kale
duniani yapata miaka milioni mbili iliyopita.
Akigusia kuhusu uhifadhi wa eneo hilo,
Waziri Mkuu alisema nako pia pajengwe kibanda cha mlinzi mwenye uwezo wa kutoa
taarifa kwa watalii na akasisitiza pia ajira hizo ziwahusu wenyeji wa eneo
hilo.
"Kwenye korongo la Frida, pawekwe
bango lenye maelezo ya Kiswahili, nako pia wapatikane vijana sita au nane,
waeleweshwe hiyo historia, wakifuzu, Wizara iwawezeshe, wapangiane zamu ya
kushinda hapo. Pia pajengwe kibanda cha wageni kupumzikia wakifika eneo hilo.
Kuhusu makumbusho ya Dkt. Leakey, Waziri
Mkuu alisema makumbusho hayo ni lulu kwa Taifa. "Ninawapongeza viongozi na
watumishi wa Mamlaka ya Ngorongoro kwa kuendeleza na kutunza makumbusho
haya."
Kwa
upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangallah
alisema kwa sasa dunia inatambua kuwa chimbuko la binadamu ni Afrika. “Hata
kama tunatofautiana sura na rangi, watu wote duniani wana asili ya
Afrika. “Kwetu sisi Tanzania, tunaadhimisha uvumbuzi huu kwa sababu fuvu
la Zinjanthropus ni alama na nembo ya
Tanzania na dunia.”
Alisema maadhimisho hayo yataendelea kwa
kufanya maonesho ya fuvu la Zinjanthropus
boisei na malikale zingine katika
mikoa sita ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Iringa, Mtwara na Dodoma.
Alisema wizara yake imebaini fursa
zilizopo kwenye sekta ya urithi wa utamaduni yaani malikale au utamaduni tuli (static
cultural heritage) na utamaduni hai (dynamic culture) ili kuvutia watilii na hivyo kuongeza idadi yao na
kuwafanya waongeze muda wa kukaa nchini (length of stay) na hatimaye kuongeza
pato la Taifa litokanalo na utalii.
“Wizara yangu imeanza kuiboresha na
kuendeleza sekta ya malikale na urithi wa utamaduni ili izalishe mazao ya
utalii na kuvutia watalii kwa kuhamisha vituo vya Idara ya Mambo ya Kale na
kuvipeleka TANAPA, TAWA, NCAA, TFS na Makumbusho ya Taifa ili viendelezwe na
kuwa vivutio vya utalii.
“Pia tumehamishia Makumbusho ya Taifa
kazi zote za uhifadhi wa urithi wa utamaduni tuli au malikale na kuanzisha
tamasha la urithi wa utamaduni wa Mtanzania (Urithi Festival: Celebrating Our
Heritage). Tamasha hili litasherehekewa Septemba, kila mwaka.
Naye Balozi wa Marekani
hapa nchini, Dk. Inmi Patterson ameipongeza Serikali kwa kukuza na kuendeleza
utalii wa kitamaduni.
Pia alisifu utajiri wa rasilmali misitu
na wa nyama ambao Tanzania imejaliwa kuwa nao. "Uamuzi wa Rais Magufuli wa
kuanzisha hifadhi ya Burigi, unazidi kunogesha sifa ya Tanzania katika suala la
hifadhi za maliasili na utalii na katika kukuza urithi na utajiri wa
nchi," alisema kwa Kiswahili fasaha.
Alisema maadhimisho hayo ni siku muhimu
kwake kwani yamewakutanisha watu wa kaliba tofauti wakiwemo wanasiasa,
wanasayansi, maprofesa kutoka Uingereza, Marekani na Ujerumani, wanafunzi
kutoka shule za Tanzania na wenyeji wa Ngorongoro.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
JUMATATU, JULAI
22, 2019.
No comments:
Post a Comment