Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Nanganga wilayani Ruangwa jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza
Afisa Elimu wa Wilaya ya Ruangwa anayeshughulikia elimu ya msingi, Bw. Selemani
Mrope atafute walimu wawili kutoka Ruangwa na kuwahamishia kata ya Nanganga
mara moja.
"Lazima kuna walimu wamejazana pale
Ruangwa mjini, leo tukitoka hapa nenda kaandike barua za uhamisho. Kesho
Jumapili, wahusika wapewe barua zao na Jumatatu waje kuripoti hapa
Nanganga," amesema Waziri Mkuu na kuamsha shangwe miongoni mwa wakazi wa
Nanganga.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumamosi,
Julai 27, 2019) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nanganga, wilayani
Ruangwa, mkoani Lindi alipopita kuwasalimia wakazi hao.
Waziri Mkuu ambaye amewasili Lindi leo
kwa mapumziko mafupi, alipokea taarifa ya shule ya msingi Nanganga ambayo
ilionesha kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 237 ina walimu sita tu. Kati ya hao,
wavulana ni 124 na wasichana ni 113.
“Shule hii ina madarasa nane likiwemo
darasa la awali, masomo yanayofundishwa ni tisa, mkibaki na walimu hawa sita,
mzigo unakuwa mkubwa kwa walimu hawa waliopo. Afisa Elimu tafuta wawili walimu
waje hapa Jumatatu, na Mkurugenzi wa Halmashauri atakupa gari ya kuwahamishia
hapa,” amesema. Shule ya msingi Nanganga, iliyoko kata ya Nanganga, iko umbali
wa km. 59 kutoka Ruangwa mjini.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa Ruangwa,
amewataka wakazi wa kata hiyo wafikirie kuanza ujenzi wa shule ya sekondari yao
ya kata ili kuwapunguzia safari wanafunzi wa kijiji hicho ambao kwa sasa
wanalazimika kwenda kusoma Nangumbu, iliyoko umbali wa km. 10.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha,
Serikali imetoa sh. milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ambayo
yakikamilika walimu watapata ofisi pia.
Amesisitiza kwamba fedha hizo zitumike
kujenga madarasa manne ambapo walimu pia watapata ofisi moja.
Pia amemwambia diwani wa kata ya Chinongwe,
Bibi Maki Camillius kwamba katika bajeti ya mwaka huu, kata hiyo itapatiwa sh.
milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za walimu katika shule ya sekondari
ya kata ya Chinongwe.
Mapema, akisoma taarifa mbele
ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Amiri Musa Kambona alisema
madarasa mawili na ofisi moja ya walimu vilibomoka mwaka 2014 kutokana na mvua
na upepo mkali na kusababisha upungufu wa madarsa na ofisi.
Akielezea changamoto nyingnea za
shule hiyo, Mwalimu Kambona alisema shule ina upungufu wa nyumba moja ya
walimu, darasa moja, matundu mawili ya vyoo vya walimu, ofisi moja ya walimu na
kukosekana kwa chanzo cha maji safi na salama kwa matumizi ya wanafunzi na
walimu.
No comments:
Post a Comment