July 25, 2019

WAZIRI MKUU ATAKA RUVUMA IONDOE VIKWAZO VYA UWEKEZAJI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Ruvuma uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo na kuondoa vikwazo vyote ili kuvutia wawekezaji zaidi.

“Mkoa wa Ruvuma kama ilivyo mikoa mingine, unazo fursa ambazo zikiendelezwa, zitaleta tija na kusaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Nitoe rai kwa mkoa uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo sambamba na kuondoa vikwazo vyovyote vya uwekezaji na biashara ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje,” amesema.

Ametoa wito huo leo mchana (Alhamisi, Julai 25, 2019) wakati akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji mkoani Ruvuma linaloendelea kwenye uwanja wa Majimaji, Manispaa ya Songea. Pia amezindua Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa huo.

Amesema katika ustawi wa uchumi, nchi nyingi hapa duniani zimeweza kukuza uchumi wao kupitia ujenzi wa viwanda na zikafanikiwa kupunguza umasikini katika jamii zao. Amezitaja nchi hizo kuwa ni Marekani, China, Japani, Korea ya Kusini na Ujerumani.

“Tunapaswa kuiga kutoka wa wenzetu. Ndiyo maana Tanzania pia tunahamasisha ujenzi wa viwanda kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mikoa ili tulete mageuzi ya kiuchumi yatakayowezesha upatikanaji wa ajira na hatimaye kuondoa umaskini,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza:

“Kongamano hili ambalo kaulimbiu yake ni “Ruvuma itavuma kwa uchumi wa viwanda, wekeza sasa,” imelenga kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo mkoani humu, na  inajipambanua vema na kuendana na azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo 2025.”

Amesema mchango wa sekta ya viwanda kiuchumi na kijamii nchini ni pamoja na kuongeza pato la Taifa na kupandisha hali ya maisha ya wananchi; kusaidia nchi isiyumbe kiuchumi ikizingatiwa kuwa viwanda vingi havitegemei hali ya hewa kama kilimo; kuboresha urari wa biashara (improve balance of trade) kwa sababu tija yake ni kubwa na hasa zikiuzwa bidhaa nyingi nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Amezitaja faida nyingine kuwa ni kuchangia maendeleo ya sekta nyingine kama za kilimo, uvuvi, elimu na madini; kutengeneza ajira kwa wananchi; kuchagiza na kuharakisha maendeleo ya teknolojia na rasilimali watu na kuwezesha matumizi mazuri ya maliasili zilizopo kwa faida zaidi.

Nyingine ni kuleta uhakika wa soko la mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini kwa sababu hutumika kama malighafi na kuwepo kwa uhakika wa kuingiza fedha za kigeni nchini kupitia mauzo ya bidhaa nje ambapo husaidia kuagiza mitambo, malighafi na bidhaa nyingine ambazo hazizalishwi nchini.

Mapema, akitoa salamu kwa niaba mabalozi wengine, Mwakilishi wa Balozi wa China, Bw.

Xian Ding alisema ana uhakika kuwa kongamano hilo litafanikiwa kuleta mabadiliko mkoani humo kwa sababu wana bidii ya kazi.

“Ninaahidi kuleta wawekezaji kutoka China kwa sababu tunataka waje kuleta teknolojia mpya, wafanye kazi pamoja na Watanzania na wawafundishe teknolojia hizo mpya. Tunataka hapa Ruvuma iwe model (mfano) kwa mikoa mingine,” alisema.

Akielezea kwa kifupi kuhusu mwongozo uliozinduliwa na Waziri Mkuu, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Hoseana Lunogelo alisema walitumia mfumo shirikishi ili kupata mwongozo unahusisha wawekezaji wa ndani.

“Mwongozo huu umezingatia Dira ya Taifa ya 2025 katika kutimiza azma ya Serikali ya kuwa nchi ya uchumi na viwanda, tumeshirikisha wananchi wa mkoa wa Ruvuma ili wasibakie kuwa watazamaji,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages