August 02, 2019

1,000 wasajili kushiriki wiki ya viwanda SADC

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya.

 Na Suleiman Msuya 
 
ZAIDI ya wafanyabishara na wamiliki wa viwanda 1,000 kutoka nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wamejisajili kushiriki maonesho ya wiki ya viwanda na kongamano.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya wakati akizungumza jijini Dar es Salaam.

Manyanya alisema mwitikio wa kujisajili kushiriki wiki hiyo ya viwanda umekuwa mkubwa jambo ambalo litachangia wiki hiyo kufana.

Alisema hadi jana asubuhi zaidi watu 1,000 kutoka nchi wanachama walikuwa wamejisali na kuthibitisha kushiriki na kwamba hadi Agosti 4 mwaka huu idadi itaongezeka.

"Hadi jana zaidi ya wafanyabiasha na wenye wa viwanda zaidi ya 1,000 wamejisajili kushiriki wiki ya viwanda ya SADC tunasikia faraja sana kuona mwitikio huo," alisema.

Naibu Waziri Manyanya aliwataka wafanyabiashara na wenye viwanda kutumia wiki hiyo kujifunza kwa wenzao iwapo yapo ya kujifunza.

Alisema iwapo wiki ya SADC  itatumika vizuri Tanzania itanufaika ziadi hivyo ni jukumu la wafanyabiasha na wenye viwanda kujipanga kikamilifu.

Alisema bidhaa zinazozalishwa Tanzania zina ubora mkubwa hivyo kinachohitajika ni kutumika kwa fursa hiyo kujitangaza.

Aidha, naibu waziri aliwataka Watanzania kuonesha ushirikiano na wageni ili waweze kutambua fursa zilizopo ili waweze kuzitumia.

"SADC ni soko kubwa lenye nchi 16 na wananchi zaidi ya milioni 300 hivyo likitumika vizuri litachochea ukuaji wa uchumi na kuchochea maendeleo," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages