August 01, 2019

MWILI WA MEJA JENERALI MSTAAFU ALFRED MBOWE WAAGWA DAR KUZIKWA KILIMANJARO

Na Mwandishi Wetu
 
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema familia imepata pigo kutokana na msiba wa kaka yake, Meja Jenerali Alfred Mbowe, aliyefariki dunia juzi.
Meja Jenerali Mstaafu Mbowe alifariki dunia Julai 28, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam akisumbuliwa na shinikizo la damu.

Amesema kaka yake huyo, mbali na kuwa kiungo muhimu katika familia pia alikuwa  msuluhishi wa matatizo  mbalimbali katika jamii.
Akizungumza katika ibada  ya kuaga mwili wa marehemu katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kunduchi Beach, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema familia inamshukuru Mungu kwa kuwapa zawadi ya Meja Jenerali Alfred (67) ambaye alikuwa kiungo muhimu na kimbilio la familia.

"Tukiwa na changamoto zozote za kifamilia au za kisiasa tumekuwa tukimwendea na kuomba ushauri wa busara na  amekuwa akitoa ushauri uliotufanikisha, hivyo ninamuomba Mungu atupatie  mtu mwingine angalau wa kushika nafasi yake" alisema Mbowe.

Akizungumza saa za mwisho alizokaa na kaka yake, Mbowe alisema : "Julai 27, mwaka huu usiku, familia iliandaa  sherehe ya kumpongeza mdhamini wa ndoa ya  marehemu Alfred kwa kufikisha miaka 60 ya, ndoa hiyo. Tulisherekea vizuri mpaka saa 7 usiku.

“Nilipotaka kuondoka kaka alinizuia na kusema "Unaenda wapi sijakaa sana na wewe muda mrefu, hivyo kaa tuongee". alisema na kuongeza:
"Nikakaa naye na akaniambia ametoa ahadi ya kuchangia ujenzi wa kanisa  huko Machame, hivyo atajitihada kumaliza kutoa ahadi hizo, lakini cha kushangaza Julai 28, mwaka huu alifariki dunia," alisema Mbowe.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema kupitia maisha ya kaka yake, aliitaka familia na jamii kwa ujumla kuwa na uvumilivu na upendo, kwani kifo hicho  ni mpango kamili kutoka kwa Mungu.

Pamoja na hayo, alisema  jamii kwa kushirikiana na viongozi  wanapaswa kuwa na umoja na mshikamano, ili kuendeleza amani nchini.
Pia Mbowe alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi mbalimbali wa serikali, dini na jamii kwa ujumla kwa kutoa msaada wa hali na mali kufanikisha mazishi ya kaka yake.

Askofu Malasusa
Akiongoza ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa  la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ) Dk. Alex Malasusa,  aliwataka waumini wa dini kuishi maisha mema ya kumpendeza Mungu.

Dk. Malasusa alisema jamii inatakiwa kujifunza kupitia maisha mema aliyoishi marehemu, kwani alikuwa mnyenyekevu, mwenye kupenda ibada na kujali jamii hadi umauti ulipomkuta.

Alisema marehemu Meja Jenerali Mbowe hakufa kwa sababu alikosa matibabu bali, Mungu aliamua kumchukua kwa makusudi yake  maalumu.
"Tutumie muda wetu vizuri tukiwa hapa duniani na  kujenga uhusiano nzuri na Mungu, ili siku  akirudi atukute tuko tayari kumlaki  kwenda katika  makao yetu ya milele," alisema Dk. Malasusa.

Pia amewataka waumini kuwa wanyenyekevu, wenye kupendana na kujali maslahi ya wengine wenye uhitaji, lakini pia kuimarisha uhusiano na Mungu.

Ibada hiyo  ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali dini na vyama vya kisiasa wakiwemo Mawaziri Wastaafu, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Waziri Mwinyi
Awali, Waziri  wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk.Hussein Mwinyi, aliwaongoza waombolezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa  marehemu Meja Jenerali Mstaafu Mbowe.

Waziri Mwinyi aliongozana na Mkuu wa Jeshi hilo, Venance Mabeyo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

Mbali na Waziri Mwinyi, walikuwapo  viongozi wastaafu mbalimbali wa Jeshi hilo ambao walifika kutoa heshima za mwisho na walipomaliza walienda kumsalimia Mkuu wa Majeshi Mstaafu David Msuguri anayeugua na kulazwa hospitalini hapo akiwa amekaa kwenye gari la kutembelea wagonjwa (Wheelchair).

Msemaji wa Familia
Msemaji wa familia, alisema Meja Jenerali Mbowe aliyekuwa namba  ya uaskari P 2877, alizaliwa Januari 6, Mwaka 1952  na kujiunga na Jeshi la ulinzi la wananchi Tanzania (JWTZ) mwaka 1973 na kustaafu mwaka 2009.
Alisema mwili wa marehemu utasafirishwa leo kwenda Machame, Kilimanjaro kwa ajili ya maziko yakayofanyika Ijumaa. Marehemu ameacha watoto watano, wakiwemo wa kike wawili. CHANZO GAZETI LA TANZANIA DAIMA
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akiongoza wanafamilia kuaga mwili wa Meja Jenerali Alfred Mbowe, ambaye ni kaka yake wakati wa ibada iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kunduchi Mtongani jijini Dar es Salaam. (Picha na Said Powa). 

No comments:

Post a Comment

Pages