November 24, 2019

FORVAC yawaita wadau kujifunza uhifadhi misitu

Mjumbe wa Kamati ya Maliasili Tarafa ya Mazingara, wilayani Handeni mkoani Tanga, Shabani Mtenguzi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uhifadhi wa misitu wanaofanya kijijini hapo. (Picha Suleiman Msuya).



Na Suleiman Msuya, Handeni

MRATIBU wa  Program ya Kuendeleza Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) Kitaifa, Emmanuel Msofe, amezitaka halmashauri na vijiji vyenye misitu kwenda kujifunza uhifadhi na endelezaji misitu wilayani Handeni mkoani Tanga.
Msofe alisema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea Msitu wa Tarawe uliopo katika Tarafa cha Mazingira wilayani humo.
Alisema Msitu wa Tarawe umejaliwa vivutio vingi huku ukiendelea kuwa msitu asili kutokana wananchi kushirikiana na halmashauri kuutunza.
Msofe alisema FORVAC imeamua kushirikiana na vijiji ili kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu hali ambayo itaweza kuwanufaisha wananchi kiuchumi, kijamii na maendeleo.
Alisema FORVAC inatamani kuona halmashauri za wilaya na vijiji vyenye misitu kutembelea na kujifunza namna ya kuendeleza rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
“Program ya FORVAC inahakikisha rasilimali misitu inakuwa na mnyororo wa thamani kwa kugusa jamii ambayo inazungukwa na misitu hiyo, hivyo nitumie nafasi hii kuziomba halmashauri na vijiji vyenye rasilimali hiyo kuja kujifunza hapa Handeni,” alisema.
Mratibu huyo amezishauri halmashauri na vijiji kutumia fursa nyingine kama vivutio vya utalii kuongeza mapato ya vijiji na halmashauri.
Msofe alitolea mfano Msitu wa Tarawe ambao una vivutio vingi kama nyoka wakubwa, pua mbili na eneo ambalo alipotea kungwi na mwali wake.
“Naomba Mratibu wa FORVAC Handeni na ofisa maliasili kushirikiana na kijiji kutangaza vivutio vilivyopo hapa Tarawe ni muhimu kwa maslahi ya wilaya na vijiji,” alisema.
Mjumbe wa Kamati ya Misitu Tarafa ya Mazingara, Shabani Mtenguzi alisema mafanikio ya uhifadhi wa misitu saba iliyopo katika tarafa hiyo yanatokana na kupatiwa elimu kuhusu faida ya rasilimali hiyo.
Alisema wananchi wamekuwa wakijitolea kuulinda misitu lakini bado kuna changamoto za vitendea kazi na majangili.
Mtenguzi aliomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza vivutio vilivyopo katika Msitu wa Tarawe ili watalii waweze kuja kutembelea.
Katibu Tawala (DAS), Wilaya ya Handeni Mwalimu Boniphace Maiga alisema alipongeza Program ya FORVAC ambayo imekuja na malengo mengi ya kuongeza thamani ya myororo wa mazao ya misitu na kuahidi kushirikiana nao.
Alisema wilaya imeweka vipaumbele vyake ambapo moja wapo ni maliasili hivyo watahakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi kuhusu maliasili zilizopo kwa kushirikiana na FORVAC.
Maiga alisema wamefanikiwa kutambua maeneo ya vivutio vya utalii kama mapango, misitu, mali kale na matukio kama ya Kibanga Kumpiga Mkoloni ambapo watayatumia kutangaza wilaya yao.

No comments:

Post a Comment

Pages