November 27, 2019

Hospitali ya Rufaa Mbeya yapigwa tafu na NMB


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila (kushoto), akipokea msaada wa vitanda vya kujifungulia akina mama kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya vyenye thamani ya Sh. Milioni 5 kutoka kwa Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Mbalizi Road, Hamadan Silliah, ikiwa ni sehemu ya msaada wa benki hiyo. (Na Mpoga Picha Wetu).

Na Mwandishi Wetu

BENKI ya NMB imetoa msaada wa vitanda, madawati na mabati vyenye thamani ya Sh. Mil. 15 katika kuboresha Sekta za Afya na Elimu mkoani Mbeya.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Meneja wa NMB Tawi la Mbalizi Road, Hamadan Silliah, alisema msaada huo umeelekezwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya ,Kituo cha Afya Iduda na Shule ya Sekondari Mwakibete.

Silliah alisema, Hospitali ya Rufaa Mbeya imepata vitanda saba, vikiwemo viwili vya kujifungulia akina mama wajawazito, magodoro na mashuka vyenye thamani ya Sh. Mil. 5.

Vifaa vingine vilivyotolewa ni pamoja na mabati na vifaa vya ujenzi kwa ajili ya Kituo cha Afya Iduda, mabati 156 na madawati 53 kwa Shule ya Sekondari Mwakibete, vyenye thamani ya jumla ya Sh. Mil. 10 na kufanya jumla ya msaada wote uliotolewa kufikia Sh. Mil. 15.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, aliishukuru Benki ya NMB kwa jitihada zao za kupambana na changamoto za kijamii, huku akiwataka wadau na taasisi zingine kuiga mfano wa benki hiyo katika kuisaidia jamii.

Awali, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Mkoa wa Mbeya, Ismail Macha, alisema kuwa msaada huo umefika kwa wakati kutokana na mahitaji na changamoto walizonazo hospitalini hapo, huku akiiomba NMB kuendelea kukubali kuwa kimbilio la jamii kutokana na changamoto zinazoikabili.

No comments:

Post a Comment

Pages