November 17, 2019

Nchi za Afrika zashauriwa kuwekeza kwenye utafiti

Na Suleiman Msuya

NCHI za Kusini mwa Jangwa la Sahara na Afrika kwa ujumla zimeshauriwa kuwekeza kwenye shughuli za utafiti ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazokabili nchi na wananchi.
Ushauri huo umetolewa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Sayansi Kanda ya Afrika ulionza Novemba 11 hadi 15 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo kumalizika, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Amos Nungu (pichani), alisema umekuwa na mafanikio makubwa kwa kada ya sayansi na utafiti kwa Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Afrika.
Alisema washiriki walisisitiza uwekezaji kwenye utafiti kama nyezo muhimu ya kuchochea maendeleo ya nchi na wananchi.
Dk. Nungu alisema utafiti unapaswa kuchukuliwa kwa uzito na sio maonesho, hivyo ili hali hiyo itokee ni lazima nchi hizo kuwekeza vya kutosha.
 “Tunahitaji uwekezaji na ushirikiano wa sisi watafiti kutoka Ukanda huu wa Kusini mwa Jangwa la Afrika ili kuepuka ufanyaji utafiti unaolenga tamanio la mfadhili na sio mahitaji ya jamii zetu,”alisema.
Alisema uwekezaji katika eneo hilo utaondoa utafiti wa kimkakati hali ambayo itamaliza changamoto za kijamii ambazo zinaibuka kila mara.
“Ili kumthibitishia mwananchi kuwa ugonjwa wa kipindupindu unachangiwa na uchafu unahitaji utafiti na sio kwenda kwa mganga wa kienyeji hivyo basi eneo hilo linahitaji uwekezaji mkubwa kuweza kubadilisha mitazamo hiyo,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema pamoja na uwekezaji kufanyika ni lazima serikali husika kuwa tayari kutekeleza matokeo ya utafiti na sio kufungua kabatini.
Aidha, Dk. Nungu alisema mkutano huo ambao ulikuwa na vikao vikubwa viwili na vidogo vitano ulisisitiza kuwepo na sayansi shirikishi na wazi kama moja ya mbinu ya kurahisha utafiti.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti Afrika Kusini (NRF), Dk. Molapo Qhobel alisema mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa kwa watafiti na nchi wanachama.
Dk. Qhobel alisema wanasayansi watafiti ndio wanaweza kutatua changamoto ya chakula, maji, afya, elimu na nyingine kupitia utafiti watakaofanya kila mtu kwa lugha yake.
“Sisi tunazungumza lugha tofauti lakini matatizo yetu yanafanana hivyo tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa changamoto zetu kama watafiti,” alisema.
Mkurugenzi huyo wa NRF alisema watafiti walioshiriki mkutano huo wameonesha dhamira ya kushirikiana kuhakikisha kuwa wanakuwa kiungo muhimu kuchangia maendeleo ya nchi na jamii zao.
Alisema iwapo watashindwa kutumia taaluma zao kutatua changamoto za jamii elimu waliyoipata itakuwa haina faida kwa jamii na kwao.

No comments:

Post a Comment

Pages