November 18, 2019

NMB yafungua tawi jipya Mbezi Louis

 MKUU wa Wilaya ya Ubungo - Kisare Makori (kushoto) na Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa Benki ya NMB - Omari Mtiga (wa pili kulia) wakifunua kitambaa kuashiria uzinduzi rasmi wa tawi jipya la NMB Mbezi Louis. Kulia ni Meneja wa NMB Kanda ya Dar es SalaaM - Badru Idd.
MKUU wa Wilaya ya Ubungo - Kisare Makori, akikata Utepe kuzindua rasmi Tawi jipya la Benki ya NMB Mbezi Louis wakati wa hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika juzi Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam - Badru Idd, Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi  wa NMB - Omari Mtiga, Katibu Tawala Wilaya ya Ilala - James Mkumbo na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Fortunata Shija.
 

Na Mwadishi Wetu, Dar es Salaam
  Benki ya NMB imefungua tawi lake jipya jijini Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa mpango wake wa kufikisha huduma za kibenki kwa Watanzania wengi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
 
Ufunguzi wa tawi hilo la NMB Mbezi Louis unaifanya benki hiyo kuwa na jumla ya matawi matano ndani ya wilaya ya Ubungo pekee. 
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa tawi hilo mwishoni mwa wiki, mkuu wa kitengo cha wateja binafsi wa NMB, Omari Mtiga, alisema uamuzi wa kufungua tawi hilo umetokana na tafiti mbalimbali zilizoonyesha kuwa Mbezi Louis ni eneo linalokuwa kwa kasi katika biashara.
“Tumeona eneo hili linakuwa kwa kasi sana kibiashara lakini wateja wetu bado wamekuwa wakilazimika kusafiri kilometa 15 wakifuata huduma zetu katika matawi ya Ubungo, Sinza, Mlimani City na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Sambamba na kauli mbiu yetu ya: Karibu Yako, tumeona tufungue tawi hapa hapa,” alisema.
Akifungua tawi hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori, alisema upatikanaji wa huduma za kibenki ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Ufunguzi wa tawi hili la NMB utasaidia kukuza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kibenki ambao kwa hivi sasa wapo chini ya asilimia 20,” alisema.
Aliipongeza NMB kwa kuja na njia za kidijiti za kufikisha huduma zake kwa Watanzania, akitolea mfano wa huduma inayowezesha watu kufungua akaunti ya benki hiyo moja kwa moja kwa kutumia simu za mkononi bila kulazimika kwenda katika tawi lolote la benki.
“Hivi karibuni, NMB imekuja na huduma inayolenga kuwahudumia waendesha bodaboda. Hii ni hatua inayostahili pongezi,” alisema Makori.
Tawi la Mbezi Louis linaifanya NMB kuwa na jumla ya matawi 224 nchi nzima.

No comments:

Post a Comment

Pages