November 16, 2019

Prof. NDALICHAKO: TUTAENDELEA KUWAHUDUMIA WAZEE

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, akiteta jambo na Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Janeth Magufuli wakati  walipotembelea makazi ya wazee Nunge, Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya wazee wanaoshi makazi ya Nunge ,Kigamboni Jijini Dar es Salaam  wakifuatilia hotuba ya waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, wakati walipotembelea kituo hicho pamoja na umoja wa wake za viongozi


Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema utaoji hudumu kwa wazee ni moja ya kipaumbele chake na kwamba itaendelea kuchukua hatua za makusudi kwa lengo la kuboresha hali za wazee na  maisha yao hapa nchini.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati alipoungana na Umoja wa Wake za viongozi wa New Millenium Women Group kutoa misaada kwenye makazi ya wazee ya Nunge yaliyopo Kigamboni jijini humo ikiwa ni sehemu ya Kumbukizi ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Umoja huo  mwaka 2009.

Waziri Ndalichako ametaja baadhi ya hatua ambazo tayari Serikali imechukua katika kuimarisha ustawi wa wazee kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Mpango wa TASAF ambao unalenga kunusuru Kaya maskini pamoja na makundi mbalimbali yanayoishi katika umaskini uliokithiri ikiwemo kundi la wazee.

Ametaja hatua nyingine zinazofanywa na Serikali  kuwa ni pamoja na kuboresha makazi ya wazee ili waweze kuishi katika mazingira mazuri

"Nunge ni moja ya kituo cha wazee ambacho serikali  imekifanyia ukarabati hivi karibuni kwa kuweka  mapaa mapya kwenye nyumba, kupaka rangi na kuweka vitanda vipya katika nyumba za wazee kwa kweli serikali inawajali wazee," alisema Waziri Ndalichako

Amesema pamoja na hatua hizo ambazo Serikali inachukua kuimarisha ustawi wa wazee hapa nchini bado jamii ina jukumu la kuwatunza wazee na watu wasiojiweza ikiwa ni pamoja na kuzingatia haki za wazee.

"Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya wazee zaidi ya milioni 2 hivyo tunapaswa kuwaenzi wazee wetu kwa sababu walijituma sana wakati wa ujana wao kututunza na kulitumikia Taifa lao," alisema Prof. Ndalichako

 Kiongozi huyo ameupongeza Umoja wa wake za Viongozi kwa kuona umuhimu wa kutoa misaada kwa wazee na kusema kuwa huo ni upendo mkubwa sana ambao umoja huo umeonesha kwa wazee wa Taifa hili.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wake za Viongozi wa New Millenium Women Group Tunu Pinda amesema Umoja huo umeona kwa kuwa ni sehemu ya jamii ni vizuri katika kuadhimisha  miaka kumi tangu kuanzishwa kwa umoja huo wakashirikiana na serikali na jamii kwa ujumla kutoa mchango wao kusaidia wazee.

Mahitaji yaliyotolewa na Umoja huo yanalenga kuwasidia wazee katika masuala ya malazi, mavazi na chakula, kuwajengea mnara wa tanki la maji utakaosaidia kusambaza maji katika nyumba zao ikiwa ni pamoja na kuezeka upya bwalo la chakula la wazee hao.

Akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake baada ya kukabidhiwa misaada hiyo mmoja wa wazee ambae hakujitambulisha  aliushukuru umoja wa wake za viongozi kwa kukumbuka wazee wa kituo cha Nunge na kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambazo imekuwa ikizifanya.

Kituo cha kulelea wazee cha Nunge kina jumla ya wazee 26  wanaume wakiwa 16 na wanawake 10.

No comments:

Post a Comment

Pages