November 21, 2019

Serikali yakiri uwepo wa changamoto ya wanawake kutomiliki ardhi nchini

Na Janeth Jovin

SERIKALI imekiri kuwa bado Tanzania inakabiliwa na changamoto ya wanawake kushindwa kumiliki ardhi hali inayochangia uwepo wa umaskini na kundi hilo kushindwa kujikwamua kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.Faustin Ndugulile wakati akizinduzi kampeni ya 'Linda ardhi ya mwanamke' inayoratibiwa na asasi za kiraia 26.

Amesema wanawake nchini wanashindwa kumiliki ardhi kutokana na mila na desturi kandamizi ambazo zinaonekana kuwa kikwazo kwao hivyo uwepo wa kampeni hiyo itasaidia kuondoa fikra hizo potovu katika jamii.

"Lazima nikiri kwamba bado nchi yetu tunakabiliwa na changamoto ya ushiriki wa wanawake katika kumiliki ardhi, lakini pia sheria zilizopo baadhi zake bado zinashida katika masuala ya umiliki wa ardhi kwa mwanawake, kwahiyo sisi kama Serikali tunaunga mkono juhudi hizi zinazofanyika kwani zina lengo la kumkomboa mwanamke na kumuinua kiuchumi," amesema.

Aidha amesema Serikali imehakikisha inaweka nyezo muhimu ya kuwasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi ili kuondokana na umaskini kwa kutenga kwenye halmashauri mikopo isiyokuwa na riba.

"Hivyo basi niwaombe wanawake wajitokeze kwa wingi kukopa mikopo hiyo isiyokuwa na riba na waitumie katika kufanya biashara,  kununua ardhi na kuziendelea, hata hivyo nawaomba mashirika muwekeze katika takwimu kwani tunahitahi ni wanawake wangapi wanamiliki ardhi kwa sasa" aseema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo, Elisante Ole Gabriel  amesema tatizo la wanawake kumiliki ardhi  bado ni kubwa hasa katika jamii ya wafugaji.

Amesema kwakuwa mwanamke akiwezeshwa kiuchumi mambo mengine anayaweza basi anashauri kuwepo kwa mpango maalum wa kuwainua na kuwaeleza utaratibu wa kumiliki ardhi ili wasidanganywe na baadhi ya wanasheria.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa kampeni hiyo, Tike Mwambipile amesema lengo la kampeni hiyo ni kufunga ombwe lililopo kati ya sera au sheria na taratibu  za maisha ya kila siku ya jamii za watanzania ikiwemo kubadili fikra za wanajamii kutoka katika mila kandamizi zinazozuia mwanamke kumiliki ardhi.

"Unaweza kwenda kijijini ukamwambia mwanamke kuwa unauwezo wa kumiliki ardhi akakataa kabisa na hiyo inatokana na mila na desturi tulizonazo ambazo nyingi zinamkandamiza mwanamke, ila naamini elimu ikitolewa wanawake watatuelewa.

"Na ndio maana tumekuja na kampeni hii ambayo italenga pia kuongeza nguvu ya haki ya wanawake kumiliki ardhi, kutoa maamuzi kuhusu ardhi na kufaidi mapato yatokanayo na ardhi," amesema

Amesema anaamini kuwa matokeo ya kampeni hiyo ni zaidi ya asilimia 60 ya wanawake wawe na uwezo wa kudai haki zao katika ardhi, kuboresha maisha ya kiuchumi, kuongeza na kuboresha upatikanaji wa ardhi kwa mwanamke.

"Tanzania imejikita katika malengo manne ambayo ni kuondoa mila na desturi kandamizi zinazo wakwamisha wanawake kupata haki zao katika ardhi, kuwawezesha wanawake kuutumia ardhi zao kwa manufaa hasa kiuchumi, kuongeza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya kutoa maamuzi,  amesema Tike.

No comments:

Post a Comment

Pages