November 20, 2019

USAJILI DIRISHA DOGO VPL SASA NI DESEMBA 16 HADI JANUARI 15

Na Salum Mkandemba

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limefanyia mabadiliko ya kipindi cha usajili wa dirisha dogo miongoni mwa klabu za Ligi Kuu Tanzania (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL), ambapo sasa dirisha hilo litafunguliwa Desemba 16.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF, kupitia Ofisa Habari wake Cliford Ndimbo, dirisha dogo la usajili kwa msimu huu wa 2019/20 litafunguliwa Desemba 16, 2019 na kufungwa Januari 15, 2020.

Kabla ya mabadiliko hayo, ilizoeleka dirisha hilo kufunguliwa Novemba 15 na kufungwa Desemba 15, huku ikielezwa kuwa litafunguliwa wakati ligi ikiwa imesimama kupisha michuano ya Chalenji inayoratibiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Senior Challenge Cup).

Michuano hiyo itakayofanyika jijini Kampala nchini Uganda, inatarajiwa kuanza Desemba 1 na kufikia ukomo Desemba 19 na kwamba baada ya kumalizika kwa michezo ya Kalenda ya FIFA, timu zitacheza raundi moja au mbili kisha ligi kusimama tena kwa karibu wiki nne.

Aidha, mchezo wa Watani wa Jadi wa soka la Bongo - Simba na Yanga utapigwa Januari 4, 2020, wiki chache baada ya dirisha dogo kufunguliwa, ikiwa na maana kuwa nyota wapya watakaosajiliwa na timu hizo, watakaribishwa na mchezo wa Mahasimu wa Kariakoo ‘Kariakoo Derby.’

No comments:

Post a Comment

Pages