November 14, 2019

Waandishi 7 wang’ara tuzo habari za sayansi

 Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti la TanzaniaDaima Suleiman Msuya, akipokea cheti cha ushindi wa shindano la tunzo ya Umahiri katika Uandishi wa Habari za Sayansi Afrika, kutoka kwa Profesa Soukeye Dine kutoka Senegali. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Africa Technology Policy Studies Network Dk. Nicholas Ozar na wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Amos Nungu. (Picha na Mpiga Wetu).

Na Mwandishi Wetu

WAANDISHI wa habari saba kati ya 24 wa vyombo vya habari, akiwemo Suleiman Msuya wa Gazeti la TanzaniaDaima, wameng’ara kwenye Shindano la Tuzo ya Umahiri katika Uandishi wa Habari za Sayansi Tanzania.
Tuzo hizo zilizoanza kutolewa mwaka 2017, zinalenga kuhamasisha waandishi wa habari kuandika taarifa za sayansi na kuhabarisha umma juu ya matokeo makubwa ya utafiti wa kisayansi.
Tuzo hizo zinazoratibiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa upande wa Tanzania na Jukwaa la Bioteknolojia za Kilimo Afrika (OFAB) zimetolewa Novemba 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia tuzo hizo za mwaka 2019 Mratibu wa OFAB Tanzania Dk. Filbert Nyindodi alisema mwaka huu kulikuwa na ushindani mkubwa na waandishi wengi walituma kazi zao.
Dk. Nyindodi aliwataja washindi wengine kuwa ni Davidi Rwenyegira kutoka Kituo cha Redio EA ambaye amekuwa mshindi wa jumla, Daniel Semberya Gazeti la Business Time na Sifuni Mshana ITV ambao watawasilisha nchi katika shindano la OFAB  likatalofanyika Novemba 21 mwaka huu jijini Mombasa Kenya.
Wengine ni Elias Msuya wa Mwananchi, Fatma Abdul wa Daily News, Benson Eustace na Msuya ambaye ni mshindi katika eneo la mwandishi anayekuja kasi katika habari za sayansi.
Alisema kazi 72 kutoka kwa waandishi 24 ziliwasilishwa katika shindano hilo ambalo linafanyika kila mwaka kwa ngazi ya taaifa na Afrika.
Mratibu huyo alisema kwa mujibu wa majaji kazi zote zilikuwa na ubora ambao unakidhi vigezo hali ambayo ilisababisha ushindani mkubwa hasa katika kumpata mshindi wa jumla.
“Kwa mujibu wa majaji washiriki wote walitimiza vigezo wamepata zaidi ya alama 65, kupata daraja B+ sio kazi ndogo. Ni ushindi mkubwa.
Bahati mbaya sheria za kombe la dunia hatua ya mtoano lazima mshindi apatikane hata kama ni kwa kurusha shilingi,” alisema.
Alisema kutokana na ushindani uliokuwepo anaona kila mshinriki ni mshindi kwa kuwa halikuwa jambo rahisi kuwapata washindi wa kwanza.
Dk. Nyindodi alisema matumaini yake ni kuona wawakilishi wa nchi katika shindano la OFAB wanaibuka washindi na kurejesha ushindi nchini.
Tuzo hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa COSTECH, Dk, Amos Nungu na washiriki wengine wa mkutano wa Baraza la Sayansi Afrika wanaomaliza mkutano wao leo.
Kwa mwaka jana mshindi wa OFAB Afrika alikuwa Mwandishi Calvin Gwabara kutoka Kituo cha Redio cha Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA).

No comments:

Post a Comment

Pages