Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akifungua jana
mkutano wa siku moja kuhusu kukuza uelewa wa masuala ya malezi na makuzi ya watoto. (Picha na Tiganya Vincent).
Na Tiganya Vincent
WANAUME Mkoani wametakiwa kuwekeza katika ujauzito wa wake zao ili kuwawezesha kujifungua watoto wenye uchangamfu na malezi na makuzi mazuri kwa ajili ya kupata wananchi bora wa baadaye.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akifungua mkutano wa siku moja wa kukuza uelewa kuhusu malezi na makuzi ya watoto.
Alisema kwa mujibu wa wataalamu malezi na makuzi mazuri ya watoto yanaanzia siku mama anapopata ujauzito na kuendelea.
Mwanri alisema hatua hiyo itawezesha mtoto kuwa mchangamfu kuanza toka akiwa tumboni na hata baada ya kuzaliwa.
“Mzazi anapaswa kuongea na mtoto wake maneno mazuri tangu akiwa tumboni na baada ya kuzaliwa kuwa naye karibu kwa kumfundisha mambo mbalimbali kwa ajili ya kumkuza katika malezi bora” alisema.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu amewataka wanajamiii kuepuka kutoa lugha za matusi na zisizofaa kwa watoto kwa kuwa zinawasababisha kujengeka katika roho ya ukatili.
“Utakuta mzazi atamtukana mtoto wake matusi mazito kama vile kichwa kama tofali…mbwa…mpumbavu ..mjinga…maneno kama hayo hayamjengi mtoto bali yanamfanya kuwa mkatili siku za usoni…tujifunze kuwaambia watoto maeneno mazuri ambayo yatawakuza katika maadili mema na kuwafanya kuwa raia wema” alisema.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Honaratha Rutatinisibwa alisema ubongo wa mtoto unakuwa tayari kupokea mambo mbalimbali yatakayokea katika maisha yake tangu siku ya kwanza anapozaliwa.
Alisema ni vema wazazi wajenge tabia ya kuongea na watoto wakiwa angali tumboni mwa mama zao na baada ya kuzaliwa ili kuwajengea uchangamfu na makuzi mema.
Mganga huyo wa Mkoa wa Tabora alisema hata wazazi wamebanwa na majukumu ni vema wakatenga muda wa kucheza na watoto wao ili kuwaongezea uchangamfu.
No comments:
Post a Comment