Na Mwandishi Wetu
Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
linamshikilia Afisa wa Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Tito Magoti (pichani).
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Lazaro Mambosasa, aliwaambia waandishi wa habari leo Desemba 20, 2019, kwamba Magoti
alikamatwa na wenzake watatu kutokana na makosa ya jinai.
Mambosasa hakueleza kwa kina juu ya
kukamatwa na Magoti, awali taarifa zilisema Magoti alitekwa saa nne asubuhi
jijini Dar es Salaam na watu ambao hawajajulikana baada ya watu hao kumkamata
kwa nguvu na kumuingiza kwenye gari lao aina ya Harrier, kisha wakaondoka naye
kuelekea kusikojulikana.
Baada ya taarifa hizo kusambaa katika mitandao
ya kijamii, Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga, alisema kwamba kabla
Magoti hajatekwa, alishuka kwenye bodaboda aliyokuwa amepanda, maeneo ya Mwenge
Kituo cha Mafuta cha Puma.
“Kwa mujibu wa mtu aliyetupatia taarifa, ni
kwamba Magoti alipotelemka kwenye bodaboda, ghafla lilikuja gari hilo ambalo
hata namba zake za usajili hazikufahamika mara moja na kuondoka naye.
“Kwa hiyo, hadi sasa tunaendelea kufuatilia
juu ya tukio hilo ili tujue chanzo cha kutekwa huko na mwenzetu amepelekwa wapi,”
alisema Henga.
Naye Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
(THRDC), Onesmo ole Ngurumwa, alisema wanasikitishwa na kutekwa kwa mwanasheria
huyo ambaye ni mfanyakazi wa LHRC.
Alisema Afisa huyo ambaye ni mtetezi wa haki
za binadamu, alichukuliwa kwa nguvu na watu wanaokisiwa kuwa ni watano, akiwa maeneo
ya Mwenge katika Kituo cha Mafuta cha Puma.
“Tukio hili lilitokea asubuhi leo
ambapo watu hao walitumia nguvu kumuingiza Magoti kwenye gari aina ya Harrier
wakiwa wamevalia mavazi ya kiraia.
“Lakini, jitihada za kumtafuta ndugu Tito,
zinaendelea ili tujue ametekwa na kupelekwa wapi.
“Kwa ujumla, mtandao wetu unasikitishwa na
kuendelea kwa matukio hayo ya utekaji kwani yameanza tena kushamiri hasa kwa
watetezi wa haki za binadamu,” alisema Ole Ngurumwa.
Katika hatua nyingine, Ole Ngurumwa alisema Jeshi
la Polisi linatakiwa kuchukua hatua za haraka na za makusudi kuhakaikisha
mtetezi huyo wa haki za binadamu anapatikana akiwa salama.
Pia, alisema watetezi wa haki za binadamu,
wanahabari na wananchi kwa ujumla, wanatakiwa kuungana kwa kupaza sauti kwa
ajili ya Magoti ili aweze kupatikana akiwa salama.
No comments:
Post a Comment