December 19, 2019

ANASWA KWA KUJIFANYA OFISA TAKUKURU

Na Tatu Mohamed
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Ilala inamshikilia Mkazi wa Mbagala, Hussein Hassan (43) kwa tuhuma za utapeli kujifanya Ofisa wa Takukuru. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Ilala, Christopher Myava, alisema pia mtuhumiwa huyo ameghushi na kujitengenezea kitambulisho namba PCCB 1565 chenye jina Hussein M. Mhando na cheo cha Principal Investigator ili aonekane kama Ofisa wa Takukuru na kufanya utapeli kinyume na sheria.

Alisema baada ya kupokea taarifa toka kwa wananchi wazalendo, kuwa mtuhumiwa huyo anatumia kitambulisho cha Takukuru katika kufanya utapeli.

"Disemba 12 tulimuwekea mtego maeneo ya Pachoto Mwananyamala, kwa bahati mbaya alikimbia baada ya kuona watu asiowafahamu karibu na gari namba T 618 DMS ambalo siku hiyo alikuwa analitumia. 

"Takukuru ilifanikiwa kulishikilia gari hilo na Disemba 16 baada ya kuona gari linashikiliwa mtuhumiwa alijisalimisha na kukiri kujifanya Ofisa wa Takukuru mwenye cheo cha Principal Investigator na kutumia kitambulisho hicho," alisema.

Aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo pia alikiri kuwa baada ya kuwakimbia maofisa wa Takukuru siku ya mtego alikimbia na kitambulisho hicho cha kughushi na kukichana ili kupoteza ushahidi.

Myava alisema kuwa uchunguzi utakapokamilika hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa kwa mujibu wa sheria. 

"Natoa rai kwa wananchi kujihadhari na matapeli wa jinsi hii. Endapo watabainika wahalifu wowote wa namna hii watoe taarifa Takukuru kupitia namba 113 simu bure ambayo inapatikana saa 24 na siku 7 za wiki ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages