December 31, 2019

Chenza adai Maafisa ugani vijijini wamekuwa bodaboda!

 Na Bryceson Mathias

KAIMU Mwenyekiti wa Mamlaka ya kuthibiti mbolea nchini, Charles Chenza (pichani), akihojiwa na ITV kwenye Kipindi cha Dakika 45, amewatuhumu Maafisa Ugani nchini walioko vijijini, akidai wamekuwa wafanyabiashara ya bodaboda badala ya kutekeleza wajibu wao ili wakulima wawe na kilimo chenye tija.
Hatua hiyo imewaudhi wengi wa  maafisa ugani waliosikia mahojiano yake na Mtangazaji wa Kipindi cha Dakika 45, Benjamini Mzinga, ambapo wamesema wao wanafanya kazi waliyoaminiwa tofauti na tafsiri potofu ya Chenza na kumtaka awaomba radhi kabla hawajachukua hatua nyingine Kitaifa.
Maafisa ugani hao waliohojiwa kwa nyakati tofauti kuhusu tuhuma hiyo na walirusha Kilio chao kwa Waziri mwenye dhamana ya Kilimo ambapo wamedai, Kiongozi huyo amewadhalirisha bila kuwa na chembe ya Ushahidi kwamba wamekuwa hawapo kwenye sehemu zao za Kazi ya kuwa waendesha biashara ya bodaboda.
Aidha wameilalamikia Serikali Kuu wakidai Kauli ya Chenza imewaondolea Ueredi na kuaminika kwao kwa Wananchi na Serikali, na hivyo hawawezi kutafuta ugomvi na kukosana na Waziri mwenye dhamana ya Kilimo au Bodi yote ya Mamlaka ya Kudhibiti Mbolea isipokuwa wanaona mbaya wao ni Chenza.
Akizungumzia uagizaji wa Mbolea, Matumizi na Mwongozo mpya wa manunuzi makubwa ya Mbolea (Bulk Procurement), Chenza akijimwambafai dhidi ya ufaniisi na matumizi mazuri ya Mbolea alijikuta akiwachokoza pasi na ugomvi maafisa ugani hao kuwa wamekuwa bodaboda.
Mmoja wa maafisa ugani alisema, wanaiomba Serikali Kuu kupitia kwa Waziri mwenye dhamana ya Kilimo kupitia mahojiano hayo kwenye kipindi hicho ili Chenza ajitathimini na kuthibitisha iwapo alikuwa na nguvu gani ya kutoa tuhuma hizo nzito dhidi yao kwa kuwajumuisha wote kama labda aliwahi kumuona moja wao na kumshitakia kwa viongozi wake.

No comments:

Post a Comment

Pages