Mbunifu
wa Mashine ya Kusafisha Fukwe, Kennedy Mwakatundu (wa pili kushoto),
akielezea namna mashine hiyo
inavyofakazi wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana. Kutoka kulia ni Mbunifu wa Kitanda cha Kubeba Wagonjwa wa
Dharura, Diana Kaijage, Kaimu Mkurugenzi wa
Idara ya Uendeshaji wa Teknolojia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH), Dk. Athuman Mgumia na Mtafiti Mtaalam wa Hakimiliki Bunifu
wa tume hiyo, Judith Kadege. (Picha na Suleiman Msuya).
Na Suleiman Msuya
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imewataka
wabunifu nchini kulinda bunifu zao ili waweze kunufaika nazo sasa na vizazo
vyao.
Hayo yamesemwa na Mshauri wa Shughuli za Ulinzi wa Miliki
Bunifu, kutoka Kituo cha Kuendeleza Uhaulishaji wa Teknolojia COSTECH Judith
Kadege wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Kadege alisema wabunifu wanapaswa kujua namna ya kulinda
bunifu zao kwa kutumia mihimili ya miliki bunifu ikiwa ni pamoja na kujua
nyenzo wanazoweza kuzitumia.
Alisema COSTECH imejipanga kuwajengea uwezo wadau tofauti
katika sekta ya utafiti na ubunifu nchini ili kuhakikisha wananufaika na
ubunifu wao.
“Elimu ya miliki bunifu inasaidia kujua haki za wabunifu kabla
ya kuanza kubuni kitu ambacho wanakifikiria, pia hapo alipobuni akitaka
teknolojia hiyo au bunifu yake itumike sehemu nyingine anatakiwa afanya kitu
kipi kabla.
Tunafundisha ili kulinda ile miliki bunifu
yake isije ikaibiwa, au ikatupwa au ikatumiwa ndivyo sivyo bila ya
idhini yake ama kibiashara au kwa matumizi mengine naamini tutafanikiwa,”
alisema.
Alisema wabunifu wengi wana mlengo wa ujasiriamali hivyo
ulinzi wa miliki bunifu utasaidia kujua wapeleke wapi bunifu ambayo imepata
ulinzi wa miliki bunifu ili iweze kufanyiwa kazi.
Mshauri huyo alisema duniani kote ulinzi wa miliki bunifu unampa
mmiliki wa bunifu uwezo wa kujua namna gani unaweza kuongea hata na makampuni
makubwa ili yatumie teknolojia husika.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendeleshaji na Uhaulishaji wa
Teknolojia katika tume hiyo, Athuman Mgumia alisema waliandaa mafunzo hayo
kwa wabunifu 60 walioshiriki na kushinda Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi na
Teknolojia (Makisato) ili kuendeleza bunifu zao.
Alisema mafunzo hayo yatawasaidia katika kuboresha teknolojia
zao na kuweza kuhakikisha kama zinawafikia walengwa wao waliowakusudia.
Kwa upande wake Mhandisi wa Mitambo Kennedy Mwakatundu,
alikiri kuwa kama wabunifu kuna vitu ambavyo hawavilindi kisheria au sheria
haiwalindi hivyo kupitia mafunzo hayo kutawawezesha kuwa na ujuzi wa kulinda
kazi zao.
Mbunifu huyo ambaye ametengeneza mashine ya kusafisha fukwe za
bahari alishauri mafunzo hayo pia yawe ni sehemu ya kuwaandaa watoto wadogo
kuweza kujua ikiwa wana kipaji.
Naye Diana Kaijage aliyebuni kitanda cha kuweka kwenye gari la
wagonjwa alisema mafunzo waliyoyapata yatawasaidia katika kulinda kazi zao
walizozifanya.
“Wabunifu tukiwezeshwa tunaweza hivyo naomba wadau wengine
kushirikiana na COSTECH kuhakikisha bunifu zetu zinatatua changamoto,”
alisema.
No comments:
Post a Comment