Grace Jackson wa JKT mshindi wa Nne km 5 akipokea zawadi.
Mshindi wa Pili km 5 Cecilia Ginoka akipokea zawadi kutoka kwa mgeni rasmi Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu.
Na Tullo Chambo, Karatu
WANARIADHA kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ),
na Klabu ya Talent ya jijini Arusha wametamba katika mbio za Kilomita 5 na 10
Tamasha la 18 la Michezo la Karatu, mkoani Arusha.
Katika tamasha hilo lililofanyika viwanja vya
Mazingira Bora mjini hapa ambako Mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili
na Utalii, Costantine Kanyasu, ilishudiwa Gabriel Geay wa Talent akitamba kwa
upande wa wanaume Kilomita 10 huku wanawake Kilomita 5 Magdalena Shauri wa JWTZ
alifanya kweli mbele ya bingwa wa mwaka jana, Failuna Matanga wa Talent.
Failuna ambaye ni mwanariadha pekee wa kike Tanzania aliyefuzu
Olimpiki Tokyo 2020, alipata upinzani mkali kutoka kwa Shauri na Cecilia Ginoka
wote kutoka JWTZ na kujikuta akikamata nafasi ya tatu.
Licha ya kujitahidi kuongoza kwa muda mrefu mbio hizo
za Kilomita 5, Failuna alijikuta akikubali yaishe mita chache kuelekea kwenye
kumaliza.
Magdalena alishinda akitumia dakika 1:40.24
akifuatiwa na Ginoka 16:5.30 huku Failuna akitumia dakika 17:19:80.
Kwa upande wa Kilomita 10 kwa wanaume, mwanariadha wa
kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay alishinda akitumia dakika 30:23:94, akifuatiwa
na Mathayo Sombi wa Talent dakika 30:43:40 na Faraja Damas wa JWTZ aKimaliza wa
tatu kwa kutumia dakika 30:45:43.
Shughuli nyingine ilikuwa kwenye mbio za baiskeli za
Kilometa 60 kwa wanaume pale Bahati Masunga wa Mwanza akiwa na baiskeli yake ya
kawaida kabisa alipowashinda washindani wenzake waliokuwa na baiskeli za
kimashindano alipoibuka wa kwanza kwa kutumia saa 1:30:33.25.
Masunga akionesha uzoefu wa watu wa Kanda ya Ziwa
kuendesha baiskeli, aliwaacha washindani wengine, akiwemo muendesha baiskeli wa
kimataifa wa Tanzania, Richard Laizer kwa dakika tatu.
Laizer alimaliza wa pili kwa kutumia saa 1:33:49:92
na mara baada ya kumaliza mbio hizo, alimpongeza mshindi kwa kumpa mkono huku
akimwambia hongera.
Kwa upande wa wanawake, mshindi alikuwa ni Esther
Laizer huku nafasi ya pili ikienda kwa Clara James katika mchezo huo wa
baiskeli kwa upande wa wanawake.
Mgeni rasmi wa ufungaji wa tamasha hilo ambaye ni
Naibu Waziri wa Maliasili na Costantine Kanyaso mbali na kuwapongeza waandaaji
alisema kuwa wengi hawaoni muunganiko wa michezo na utalii, lakini kuna
uhusiano mkubwa wa vitu hivyo viwili.
Alisema tamasha kama hilo linatoa linasaidua kutoa
nafasi za kuibua vipaji vingi na kuwa mchango mkubwa katika sekta ya michezo
nchini, lakini kinachotokea mashindano kama hayo yanapoandaliwa hakuna
muendelezo wa vipaji, ambapo alishauri kuwa vipaji hivyo viendelezwe.
Alisema klabu za michezo ni chache sana nchini
tofauti na nchi zingine, ambazo uwa na matamasha mengi ya michezo kama hayo, ambayo
yamekuwa msaada mkubwa sana katika kuendeleza michezo katika nchi zao.
No comments:
Post a Comment