HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 16, 2019

KATIBU MKUU MWALUKO ATAKA MIPANGO KABLA YA MAAFA NA SIO WAKATI WA MAAFA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko akisisitiza jambo wakati wa kikao cha Jukwaa la Taifa la Usimamizi wa Maafa nchini leo jijini Dodoma, tarehe 16 Desemba, 2019.kulia kwake ni Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, Ofisi ya Waziri Mkuu, Meja, Selestine Masalamando.

  
Na OWM, DODOMA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko amelielekeza Jukwaa la Taifa la Usimamizi wa Maafa nchini kutoa ushauri wa kitaalamu unaojikita katika hatua ya kabla ya maafa kutokea na sio kujikita wakati wa maafa yanapotea kama ilivyozoeleka, kwa kuwa ushauri wa namna ya kuzuia na kujiandaa na maafa kabla ya maafa kutokea huweza  kupunguza madhara ya maafa na rasilimali zinazohitajika katika upunguzaji wa madhara hayo.

Ameyasema hayo leo Jijini Dodoma, wakati akifungua kikao cha Jukwaa hilo ambapo amebainisha kuwa wakati wa kukabili majanga na maafa kunakuwepo na mipango mingi ambayo hutekelezwa na wadau wa menejimenti ya maafa na kwa uchache wakati wa urejeshaji hali wa maafa,  lakini mipango ya kujiandaa na  kuzuia maafa ambayo hufanyika kabla ya maafa kutokea  kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara ya  maafa yatakapotokea huwa haitekelezwi.

“Tumekuwa na maafa hapa nchini ambayo yameleta madhara nchini,  itakumbukwa ajali ya moto mjini Morogoro hivi karibuni, tujiulize kuna mipango inayoendelea katika kuzuia majanga hayo, yapo maafa ya mvua yanaendelea kutokea,  lakini je ipo mipango ya kabla ya maafa kutokea, lakini pindi maafa yakitokea wadau wa menejimenti ya maafa hujitokeza na kuanza kukabili maafa, sasa nataka nguvu nyingi ielekezeni kwenye mipango ya kabla ya maafa kutokea na hata ikibidi ainisheni majanga yanayoweza kutokea kwenye maeneo husika ili jamii iweze kujiandaa na kuyazuia maafa husika kabla yakutokea“ Amesisitiza Mwaluko.

Aidha, amelielekeza Jukwaa hilo kuupitia Mkakati wa Taifa wa Kupunguza athari za maafa na kuhakikisha kuwa unaendana na uhalisia wa hali ya majanga yanayotokea katika jamii ili uweze kutekelezeka kwa kuweka malengo yenye uhalisia, huku akisisitiza kuwa ni vyema mkakati huo ukatafsiriwa kwa Kiswahili ili uweze kutumiwa vyema na walengwa kuanzia ngazi ya msingi ya maafa ambayo ni kamati za vijiji.

Katika hatua nyingine Bi. Mwaluko  amelielekeza Jukwaa hilo kuwa na ushirikiano miongoni mwa wadau wa jukwaa hilo kwa kila mdau kuainisha majukumu yake na namna anavyoyatekeleza majukumu yake, ili kuweza kujua jukumu la kila mdau na anafanya nini  na kwa wakati gani na hatimaye mipango ya kuimarisha Usimamizi wa maafa iwe inayotekelezeka.

“Kupunguza madhara ya maafa ni suala mtambuka lenye mchango mkubwa katika shughuli za maendeleo.Wakati mwingine wananchi wamekuwa wakipata madhara kwa kukosa uelewa hivyo ni vyema kila mdau kuwajibika katika majukumu yake kwa kutoa fursa ya uratibu wa usimamizi wa maafa kwa ushirikiano  wa wataalamu wa  fani mbalimbali” Amesema , Bi. Mwaluko

Awali akiongea katika kikao hicho, Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Maafa , Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, ameeleza kuwa Jukwaa hilo ni chombo cha kisheria ambacho lipo kwa ajili ya kutathmini na kutoa ushauri wa kitaalam kwa serikali kuhusu majanga ya aina zote, ambapo Jukwa hilo  linaundwa kwa kuzingatia Kifungu cha 40 cha Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na.7 ya mwaka 2015.

Jukwaa hilo ambalo linajumuisha wataalamu wa fani mbali mbalimbali  kwa kujumuisha sekta ya umma na sekta binafsi, mashirika ya kimataifa na umoja wa mataifa na asasi za kiraia jukumu lake la  msingi ni kutoa ushauri maeneo ya kipaumbele katika usimamizi wa maafa kwa uratibu na ushirikishawaji wa wadau ili kufanikisha kujumuisha upunguzaji wa madhara ya maafa katika mipango na sera za maendeleo ya taifa na katika misaada ya kibinadamu.

No comments:

Post a Comment

Pages