December 07, 2019

MRADI WA KUFUA UMEME RUSUMO KUKAMILIKA 2020

 Waziri wa Nishati wa Tanzania, Medard Kalemani, akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali huku akiwa ameambatana na mawaziri wa Rwanda na Burundi.
Eneo la kufua umeme likiendelea kujengwa.


Na Alodia Dominick, Kagera

Mradi wa kufua umeme wa maji unaojengwa Rusumo wilayani Ngara mkoani Kagera umefikia asilimia 59 ya ujenzi wake tangu umeanza mwaka 2017.Mradi huo unaziunganisha nchi tatu za Rwanda, Burundi na Tanzania, akitoa maendeleo ya mradi huo katika mkutano wa 11 Mwenyekiti wa Mawaziri wa nchi tatu za Rwanda, Burundi na Tanzania zitakazonufaika na mradi huo Waziri wa Nishati hapa nchini, Medard Kalemani, amesema tangu mradi huo umesainiwa mkataba ni miezi 36 sawa na miaka mitatu ambapo ulianza Februari 2017.

Waziri Kalemani ameongeza kuwa maendeleo ya mradi ni mazuri kwani baada ya kuona asilimia ulipofikia ambazo ni 59 mawaziri hao wameona kuna hali nzuri ya ujenzi wa mradi huo.

“Baada ya kuwa tumekagua miundo mbinu ya ujenzi katika mradi huu mimi na mawaziri wenzangu tumeridhishwa na maendeleo ya mradi huu na tumejipa matumaini kuwa mwisho wa mkataba ambao ni mwaka kesho mradi utakuwa umemalizika na wananchi wa nchi zetu tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi wataanza kunufaika na umeme huu”. Amesema Waziri Kalemani.

Ameendelea kueleza kwamba, mawaziri hao wamefanya ukaguzi wa miundo mbinu mbalimbali zikiwemo majengo ya wataalamu ambayo yako hatua za mwisho, kituo cha kufua umeme kilichopo upande wa Tanzania ambacho kinakaribia hatua za mwisho kukamilika na eneo ambapo utawashwa umeme ambalo liko katika nchi ya Rwanda.

Kwa upande wa waziri wa Nishati na Migodi kutoka nchini Burundi Claver Gatete amesema wamemtaka mkandarasi kufanya tathimini upya ya upasuaji wa miamba kutokana na upasuaji wa miamba kuathiri nyumba za wananchi ambao wako karibu na mradi.

Naye Waziri wa Miundombinu katika nchi ya Rwanda, Come Manirakiza, ameshukuru mawaziri wa nchi ambazo zinashirikiana kuhakikisha mradi unajengwa na kwa muda uliopangwa na jinsi wanavyojitahidi kuufuatilia kwa karibu ili ulete manufaa kwa wananchi wa nchi hizo tatu.

Hata hvyo mradi huo utagharimu dola milioni 468 na utazalisha umeme wenye megawati 80 ambao utategemea maji kutoka mto Kagera unaoziunganisha nchi hizo.

No comments:

Post a Comment

Pages