December 11, 2019

'Ndoa' ya CRDB, TTCL kunufaisha wengi

Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa (katikati), akishuhudia uzinduzi wa huduma ya kuhamisha fedha kati ya SimBanking na T-Pesa uliofanywa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa benki hiyo, Stephen Adili (kushoto) na Mkuregenzi wa T-Pesa, Lulu Mkude. (Na Mpiga Picha Wetu). 


Na Irene Mark

BENKI ya CRDB na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), wamezindua mpango wa pamoja kupitia huduma za SimBanking na T-Pesa utakaowawezesha wateja kupata huduma za kifedha kwenye simu zao za mkononi.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa alisema mpango huo unalenga kuwarahisishia wateja huduma za kuhamisha fedha kutoka akaunti za CRDB kwenda T-Pesa, kuhamisha fedha kutoka T-Pesa kwenda akaunti yoyote ya CRDB na kununua muda wa maongezi kwa Simbanking.

“Lengo letu ni kuwapa wateja wetu uzoefu bora zaidi pindi watumiapo huduma ya SimBanking. Tunataka kuona mteja akiingia kwenye SimBanking USSD kwa kupiga *150*03# au SimBanking App anamaliza mahitaji yake yote ya kifedha ‘One Stop Shop’ ikiwamo miamala ya T-Pesa,” alisema Raballa.

Raballa alisema ushirikiano huo na TTCL utataidia kusogeza huduma kwa watanzania wengi zaidi hususani maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa Raballa, takwimu zinaonyesha ni asilimia 60 ya watanzania ndio wameunganishwa na mfumo wa kifedha kupitia simu za mkononi, wakati ni asilimia 17 tu ya watanzania ndio wanaotumia huduma za kibenki.

“Benki ya CRDB inafanya kazi kwa bidii kuhakikisha watanzania wengi wanapata huduma za kifedha, hatua ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wetu.

"...Tunafurahi sana kushirikiana na TTCL katika kufanikisha azma hii," Raballa.

Mkurugenzi Mtendaji wa T-Pesa, Lulu Mkude, alisema ushirikiano huo ni mafanikio  kwa TTCL, kwani utawawezesha maelfu ya watanzania wote wa mijini na vijijini kupata huduma za kifedha za kwa urahisi.

Lulu alisema TTCL kuunganishwa kwa huduma ya T-Pesa na SimBanking kutawasiaidia wateja wa Benki ya CRDB kuweka pesa kwa urahisi kwenye akaunti zao kupitia T-Pesa lakini pia kuongeza salio au kuwatumia ndugu jamaa na marafiki fedha kwenye akaunti zao za T-Pesa.

''Kufurahia huduma mteja atatakiwa kuingia katika menu ya T-Pesa kwa kupiga *150*71#, na kisha kuchagua huduma ya SimBanking,” alisema Lulu Mkude

Benki ya CRDB ni taasisi binafsi ya fedha inayoongoza nchini Tanzania tangu mwaka 1996 ilipoanzishwa.

Benki ina kampuni tanzu mbili ambazo ni Benki ya CRDB Burundi na CRDB Bank Insurance Brokers Ltd.

Benki inatoa huduwma tofauti kupitia mtandao wake wa matawi 238; mashine 552 za kutolea fedha (ATM), matawi 15 yanayotembea, mawakala 10,815 na vituo 1,184 vya mauzo.
 

No comments:

Post a Comment

Pages