December 28, 2019

Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika niya Kimataifa

Afisa Utamaduni Bw.Christopher Mhongole anayemuwakilisha Mratibu wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika (wa kwanza kulia) akimwonesha kwa nje Ukarabati unaondelea wa Jengo lilokuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi wa Bara la Afrika, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Ally Possi (wa kwanza kushoto) alipofanya ziara katika ofisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.


Na Anitha Jonas – WHUSM
 
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Ally Possi aagiza Idara ya Maendeleo ya Utamaduni na Mratibu wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kuhakikisha wanarasimisha Programu ya Urithi wa Ukombozi Bara la Afrika.

Dkt. Possi ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika Ofisi ya Mratibu wa Programu ya Urithi wa Ukombozi Bara la Afrika kwa lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa Programu hiyo pamoja na kufahamu mpango wa kuiendesha.
 
“Kaeni pamoja na muandae Mpango Mkakati pamoja na Maandiko ya kuomba Ufadhili wa Programu na mpango huo uwe unatoa dira ya namna Programu itatekelezwa sababu niyakimataifa na siyo wa Tanzania pekee kwani kuna nchi za Afrika zinahusika na nchi za ulaya hivyo ni vyema kuwa na mpango madhubuti wa utekelezaji wa Programu hii,”alisema Dkt. Possi.

Akiendelea kuzungumza Dkt.Possi alisistiza kuwa kwanza Mratibu wa Programu anapaswa kuwa na Kanzi data ya Mawasiliano ya kila nchi iliyohusika katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika kuanzia katika ngazi za Kitaifa mpaka Kimataifa na hii
itarahisisha utekelezaji wa shughuli za programu na usambazaji wa taarifa.

Pamoja na hayo nae Kaimu Mratibu wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika Bw.Christopher Mhongole alieleza kuwa programu inamalengo makuu manne ambayo mojawapo ni Kuamsha Tafiti za Ukombozi wa Bara la Afrika,Kuenzi Mashujaa waliyopigania Uhuru pamoja na Kuratibu Programu kwa kushirikiana na nchi wanachama.

Aidha, Bw.Mhongole alieleza pia Programu hiyo ilianza kuratibiwa na Wizara kuanzia mwaka 2011 na shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwemo ukusanyaji wa taarifa
mbalimbali za wapigania uhuru wa kitaifa pamoja na ukusanyaji wa nyimbo mbalimbali zilizokuwa zikizungumzia harakati ya ukombozi wa Bara la Afrika.

Halikadhalika nae Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Bw.Boniface Kadili alikiri kupokea melekezo ya Kaimu Katibu Mkuu huyo na kueleza kuwa Idara
itakwenda kuyafanyia kazi.

No comments:

Post a Comment

Pages