Wizara ya Fedha na Mipango inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyoandikwa kwenye gazeti la Mtanzania toleo la tarehe 18/12/2019 yenye kichwa cha habari “Wastaafu EAC waibuka na mafao yao” ambapo taarifa hiyo ilieleza kuwa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki hawajalipwa mafao yao kwa miaka 40 iliyopita.
Wizara ya Fedha na Mipango inapenda kuufahamisha Umma kuwa imekwishawalipa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mujibu wa “Hati ya Makubaliano” (Deed of Settlement) iliyosajiliwa Mahakama Kuu tarehe 21/09/2005, kati ya Serikali na watumishi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hati ya Makubaliano ilibainisha wazi mambo yafuatayo:-
(i) Wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walikubali kufuta madai yao
yote yaliyokuwa katika Kesi Na. 95 ya mwaka 2003, waliyoifungua Mahakama Kuu ya Tanzania;
(ii) Serikali ilikubali kuwalipa wadai wote waliokuwa wamefungua kesi mahakamani na
wengine wote waliofanya kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla ya Juni 30, 1977, na baada ya malipo hayo kufanyika, Serikali isingedaiwa tena;
(iii) Serikali ilikubali kuwalipa wastaafu 31,831 jumla ya shilingi 117.0 bilioni kwa misingi ya stahili ya kila mmoja kulingana na taarifa ya kila mmoja wao kwenye jalada au nyaraka nyingine zilizothibitishwa. Aidha, Serikali ilikubali kuchukua gharama za mawakili wa wadai ili malipo wanayolipwa wastaafu hao yasikatwe chochote.
Zoezi la ulipaji mafao kwa ujumla lilikamilishwa mwaka 2009/2010 na serikali iliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuendelea kushughulikia madai halali yatakayojitokeza, hususan yale yanayohusu mirathi kwa wahusika katika zoezi hili (case by case basis) kwa kutumia Sheria na taratibu zilizotumika katika zoezi husika. Hadi Desemba 2013 jumla ya wastaafu 31,788 kati ya 31,831, walikwishalipwa kiasi cha Shs 116,880,813,918.39 ikiwa ni sawa na asilimia 99.9 ya fedha zote zilizokubalika kulipwa.
Kwa maelezo haya Serikali kwa mara nyingine tena inarejea kusisitiza kuwa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamelipwa haki zao zote kwa mujibu wa sheria na inatoa wito kwa wastaafu wote wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kukubali kuwa malipo yaliyolipwa baada ya
uhakiki ni halali kwa mujibu wa sheria.
Kwa kuwa Serikali inatoa kipaumbele kwa maslahi ya watanzania wote hususan wanyonge, hata mara baada ya kuwa imelipa mafao hayo, bado imefungua mlango wa kupokea na kuendelea kusikiliza madai ya mtu mmoja mmoja na kulipa baada ya kujiridhisha na uhalali wa madai husika.
Aidha, Serikali inawasihi sana wazee wetu hawa kujiepusha na upotoshaji na udanganyifu kutoka kwa wajanja wachache wanaotaka kujinufaisha kupitia migongo yao kwa kuendelea kujidai kwamba wao wana uwezo wa kusimamia madai yao ambayo hayapo.
metolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
DODOMA
20 DISEMBA, 2019
No comments:
Post a Comment