Na Betty Kangonga
WAKULIMA Nchini wametakiwa kujiunga katika vikundi ili kuhakikisha wanakata bima ya kilimo hatua itakayoweza kuwainua kiuchumi.
Akizungumza
mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam kwenye mafunzo ya uelewa wa
Bima kwa wanahabari, yaliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Bima (TIRA),
Mshauri wa masuala ya bima, Eliya Kajiba, alisema kuwa hadi sasa ni
kampuni tano tu ndizo zinazokata bima hiyo.
Kajiba
alisema, bima hiyo ni mpya na bado haitambuliki kwa wakulima wengi
hivyo kuna umuhimu wa kutoa elimu ili kuhakikisha sekta hiyo inajiunga
na matumizi ya bima hiyo.
“Bima
hii ni mpya sana kwa wakulima na hasa katika uchumi huu wa viwanda huku
mahitaji yake yakiwa ni makubwa kwa sasa,” alisema.
Mshauri
huyo alisema, bima hiyo inakinga upungufu wa mavuno unaosababishwa na
ukame, mvua iliyozidi (mafuriko) na magonjwa ya mimea.
Hivi
karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Tira, Dk. Baghayo Saqware, alisema kuwa
hadi sasa kati ya kampuni 29 za bima zilizopo taarifa zinaonyesha ni
chini ya tano zinatoa bima hiyo.
Dk. Saqware alisema, tayari wadau muhimu wamejulishwa kuhusu mkakati huo wa kufidia hasara wanayoweza kupata wakulima.
Alisema
kuwa wakulima watafidiwa kwa mfumo unaotumika duniani ambapo kuna aina
mbili ambayo ni weather index (bima ya majanga ya hali ya hewa) au
(bima ya mavuno).
Mkurugenzi
Mkuu huyo alisema kampuni za bima hulipa fidia pia katika majanga
mengine ya kibinadamu akitolea mfano moto au uvamizi wa mifugo
mashambani.
“Bila kujali
sababu, bima italipa kulingana na uharibifu uliotokea, kama mkulima
katumia mbegu bora, akapanda vizuri na kwa wakati na kufuata viwango
vyote vinavyoshauriwa huku akiwa na matarajio ya kuvuna magunia 20 kwa
mfano lakini akaambulia magunia pungufu, hapo bima itamlipa kiasi
kilichopotea,” alisema.
Hata
hivyo ilielezwa kuwa kampuni za bima zinasema kuwa kikwazo cha
kushindwa kutoa bima ya kilimo ni kukosekana kwa taarifa na wakulima
kushindwa kujiunga kwenye vikundi ambavyo ni rahisi kuvihudumia.
No comments:
Post a Comment