December 11, 2019

TPSF YAZINDUA MFUMO WA NFLIP

NA FARAJA EZRA 

JUKWAA la wafanyabiashara kutoka Sekta binafsi (TPSF) kwa kushirikiana na Serikali wamezindua mfumo mpya wa Kielekroniki (NFLIP) utakaosaidia kuwapunguzia gharama za usafirishaji wa mizigo inayotoka na kuingia nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Miradi ya Uendeshaji wa Biashara nchini Edward Furaha, alisema mfumo huo utarahisisha  Usafirishaji  wa mizigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Aidha Furaha alisema Mfumo huo unaitwa 'National Freight Logistics Informations Portal' (NFLIP) na utakuwa mahususi kuratibu mchakato wa usafirishaji wa mizigo.

Alisema mfumo huo awali wasafirishaji walikuwa wakisafirisha mizigo kwa muda mrefu na madereva walikuwa wakipata usumbufu hasa katika bandari sehemu ya mawasiliano kati ya mfanyabiashara na mnunuaji mzigo, hivyo mzigo kukaa kwa muda mrefu bandarini.

Furaha alisema Tanzania ni Nchi pekee iliyozungukwa na Nchi 6 zisizokuwa na Bandari hivyo kuzinduliwa kwa Mfumo huo utasaidia kuwavutia Wawekezaji, Wafanyabiashara waliokuwa wakitumia bandari na jambo ambalo litasaidia kuongezeka kwa  pato la Taifa.

Alifafanua kuwa  mfumo huo  utarahisisha kupunguza gharama katika soko zima la usafirishaji mizigo na Utatumika nchi nzima na kwa upande wa  wasafirishaji kutoka nje unapatikana mtandaoni.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Simba Group Azim Dewji, alisema licha ya changamoto wanazopitia wafanyabiashara bado wanaendelea kuishukuru serikali  kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo viwanja vya ndege, Bandari, Reli, na barabara.
Aidha Dewji alisema  hiyo ni ishara ya kuona kuwa serikali ina mapenzi mema na ya kuwasaidia wananchi wake lengo likiwa kukuza nankuinua uchumi wa viwanda.

Pia amewataka madereva  wanaosafirisha mizigo nje ya nchi kuwa mabalozi wema wanapofanya mawasiliano kwani wamebeba utambulisho wa taifa la Tanzania.

"Madereva wengi wanapojitambulisha mara nyingi wanatoa kauli ambayo haina staha kwa jamii husika hivyo tunatafsiriwa  kwa mtazamo hasi, ndiyo maana nimetoa msisisizo kuwa wawe mabalozi wema," alisema Dewji.

Alisema sekta binafsi ikishirikiana vema na serikali katika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji hakika uchumi wa kati unapatikana kwa urahisi.

No comments:

Post a Comment

Pages