December 13, 2019

Ufundi Stadi Kufundishwa kwa Lugha ya Kiswahili

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu, akisisitiza jambo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Mitaala na Mihtasari hiyo leo, tarehe 13 Desemba 2019 katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam.
 
Na Tatu Mohamed

KATIKA kuendelea kupanua wigo na fursa za upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetafsiri Mitaala ya fani 24 na Mihtasari 16 katika lugha ya Kiswahili.

Mitaala na Mihtasari hiyo imekabidhiwa rasmi leo Desemba 13, 2019 kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Ave Maria Semakafu, na inatarajiwa kuanza kutumika kufundishia ufundi stadi katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) nchini. 

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam, Dk. Semakafu ameipongeza VETA kwa kukamilisha kazi hiyo na kusema kuwa ufundishaji kwa Kiswahili kutawawezesha wananchi wengi, kujifunza na kuelewa vyema mafunzo hayo.

Amesema, wapo watu wengi walioamua kujifunza ufundi stadi katika mfumo usio rasmi kwa sababu ya changamoto ya lugha inayotumika kufundishia, kwani wengi wao wana ugumu kufuatilia vyema mafunzo yanayotolewa kwa lugha ya Kiingereza.  

"Tunakwenda kwenye Uchumi wa Viwanda. Inabidi tukubali kubadilika. Matumizi ya Mitaala ya Kiswahili iwe hatua ya kwanza. Kuna mengi ya kuboresha. Tufungue milango ili tupokee mawazo mapya na kuyafanyia kazi. Ufundi Stadi uwe mkombozi kwa jamii nzima ya Watanzania, hata wanaoendesha shughuli zao za kifundi mitaani,” amesema Dk. Semakafu.

Aidha ameishauri VETA kuchambua na kuona kama kuna haja ya kuwa na kundi la wale wanaotaka kujifunza kwa Kiingereza kwa lengo la kuendelea na masomo ya juu zaidi, lakini mafunzo ya jumla yatolewe kwa lugha ya Kiswahili. 

Awali akitoa taarifa kwa Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Pancras Bujulu amesema jumla Mitaala 24 na Mihtasari 16 imetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, ambapo nakala 240 zimechapishwa kwa kila kitabu, hivyo kufanya jumla ya nakala za Mitaala na Mihtasari zilizoshachapwa kuwa 9,600.

No comments:

Post a Comment

Pages