December 11, 2019

Wanahabari wapewa mafunzo ya nishati jadidifu

 Baadhi ya Wakufunzi na Waandishi wa habari wanaoshiriki katika mafunzo ya nishati jadidifu.
 Mkufunzi Daniel Mwingira kutoka Nukta Africa akiwasilisha mada ya kupambana na habari za uzushi na upotoshaji.
 Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulacvk Dausen.
Mwandishi wa Habari wa Highlans FM, ya jijini Mbeya.


Na Happeniss Mnale

MKURUGENZI Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), John Chikomo, amewataka waandishi wa habari wanaohudhuria darasa maalum la nishati jadidifu kutumia vizuri mafunzo ili kubobea na kuifaidisha jamii.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua darasa hilo, Chikomo, alisema mafunzo hayo maalum ya miezi sita yanalenga kumsaidia mwanahabari kuzalisha habari za nishati kwa ubora.

Chikomo alisema, mafunzo hayo pia yatasaidia kuboresha habari ambazo zitakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen, alisema mafunzo ya nishati jadidifu ni fursa kwa wanahabari na vyombo vya habari kuboresha maisha ya Watanzania na kuongeza kipato.

Dausen alisema darasa hilo pia litawezesha wanahabari kutotegemea maudhui kutoka kwenye makampuni na mashirika.

Aidha alisema darasa hilo litafungua mlango wa kufahamu njia mpya za kuandika habari zikiwemo za takwimu na uthibitishaji habari.

Mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, Daniel Mwingira, amewafundisha waandishi wa habari namna wanavyoweza kutumia zana ya ‘Advance Google search’katika utafutaji wa vitu mtandaoni na uthibitishaji habari kama njia mojawapo ya kupambana na habari za uzushi na upotoshaji. 

Mmoja wa waandishi wa habari kutoka Mbeya, Samwel Ndoni, alisema mafunzo hayo yatamsaidia kuandika habari za uhakika ambazo haziwezi kumuingiza kwenye migogoro kwa kuwa zitakuwa zimethibitishwa.

Mafunzo hayo ya miezi sita yamefadhiliwa na Shirika lisilo la kiserikali Hivos, Nukta Africa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET).

No comments:

Post a Comment

Pages