December 10, 2019

WANASAYANSI WA TAFITI RASILIMALI VITU WATAKIWA KUFANYA TAFITI ZENYE TIJA KWA WANANCHI

Na Ahmed Mahmoud, Arusha

Wanasayansi Afrika wametakiwa kufanya tafiti zenye kuleta mslahi ya nchi katika uchumi wa kati na zenye kujibu changamoto za wananchi katika mali ghafi na rasilimali vitu ili bara la Afrika liweze kusonga mbele kimaendeleo kuliko hivi sasa kwa kuwa bara hili ni masikini pamoja na kuwa na mali ghafi na rasilimali nyingi kila kona.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi,Teknolojia na Mafunzo na Ufundi,William Ole Naasha wakati akifungua Kongamano la Jumuiya ya Wanasayansi watafiti wa mali ghafi na rasilimali vitu Afrika lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Cha Nelson Mendela kilichopo Mkoani Arusha na kushirikisha wanasayansi kadhaa duniani.

Naasha alisema Bara la Afrika ndio linaloongoza kwa kuwa na mali ghafi na rasilimali nyingi lakini ndio bara pekee masikini duaniani hivyo ni wajibu wa wanasayansi kufanya utafiti wa mali ghafi na rasilimali vitu ili wananchi wa bara hilo waweze kunufaika rasilimali zilizowazunguka.

Alisema na kuwataka wanasayansi kufanya tafiti zenye kujibu changamoto zinazowazunguka wananchi na kupata majibu sahihi ili bara la Afrika liweze kuendelea na kutoka katika umasikini wa kupindukia uliopo sasa.

Waziri alisema kwa hapa nchini wanasayansi wanahitajika sana kwa sasa katika sera ya serikali ya awamu ya tano ya Rais Dkt John Magufuli ya Uchumi wa Viwanda na Uchumi wa Kati ili waweze kufanya tafiti mbalimbali za mali ghafi na rasilimali vitu na kutoa majibu sahihi za kuondoa changamaoto za wananchi.

Alisema wanasayansi wenyewe wa hapa nchini ndio wanaoweza kufanya tafiti za mali ghafi na rasilimali na sio kungojea wanasayansi kutoka nchini.

‘’Tufanye tafiti zinazotatua changamoto ndani ya nchi ili tutokea katika dimbwi la umasikini kwani Bara la Afrika ni tajili lakini tunashindwa kutumia ipasavyo mali ghafi na rasilimali watu zilizopo’’alisema

Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho,Prf Emmanuel luoga alisema kuwa kongamano kama hilo linasaidia katika kuleta elimu mpya katika masuala ya kitafiti kwani wanasayansi waliobobea kutoka katika kila pembe ya dunia wamewasili katika kongamano hilo kujadili mambo mbalimbali ya kitafiti katika Bara ya Afrika.

Prf Luoga alisema baada ya kongamano hilo wanasayansi wa Afrika wanaweza kupata kitu kipya zaidi katika shughuli za kitafiti lengo ni kutaka mali ghafi na rasilimali iliyopo katika Bara la Afrika kunufaisha wananchi wake.

Alisema wanasayansi waliobobea kutoka katika nchi zilizoendelea duniani wamekuja katika kongamano hilo lengo ni kutaka kuwapiga msasa wanasayansi wa Afrika kufanya tafiti zenye kujibu changamoto kwa wananchi na zenye manufaa kwa kwa jamii na sio vinginevyo.

Naye Rais wa Jumuiya hiyo,Prf Hulda Swai alisema kuwa jumuiya hiyo ina zaidi ya miaka 21 na kila baada ya miaka miwili wanasayansi wa jumuiya hiyo hukutana na kila mmoja hutakiwa kuja na suluhisho la tafiti alilofanya kwa maslahi ya wananchi wa Bara la Afrika.

Prf Swai alisema Bara la Afrika ni bara lenye utajili mkubwa wa mali ghafi na rasilimali vitu na kutoa mfano wa nchi ya Kidemokrasia ya Kongo{DRC} lakini wananchi wake ni masikini wa kupindukia hivyo ni wajibu wa wanasayansi kufanya tafiti za kina na kuja na majibu yenye kuleta suluhisho kwa jamii kunufaika na mali ghafi na rasilimali vitu.

No comments:

Post a Comment

Pages