January 07, 2020

KAHATA MCHEZAJI BORA MWEZI DESEMBA

KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, Francis Kahata amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Desemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2019/20, huku Boniface Mkwasa wa Yanga akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo. 

Mkwasa na Kahata walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). 

Kwa mwezi huo wa Desemba, Simba ilicheza michezo mitatu, ikishinda yote, iliifunga Lipuli mabao 4-0, ikaifunga KMC mabao 2-0 na pia ikaifunga Ndanda mabao 2-0, huku Kahata akiwa sehemu kubwa ya mafanikio ya Simba kwa mwezi huo na alikuwa katika kiwango bora ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili na kutoa pasi za mwisho moja. 

Kahata aliwashinda Hassan Dilunga wa Simba na Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union alioingia nao fainali, ambapo Dilunga naye alikuwa sehemu ya mafanikio hayo ya Simba akifunga mabao mawili na kutoa pasi ya mwisho moja, wakati Mwamnyeto alitoa mchango mkubwa kwa Coastal Union iliyocheza michezo miwili na kushinda yote, ikiifunga Azam FC bao 1-0, kisha ikaifunga Mbeya City mabao 2-0. 

Kwa upande wa Mkwasa aliwashinda Juma Mgunda wa Coastal na Sven Vandenbroeck wa Simba, ambapo Mkwasa aliiongoza timu yake katika michezo minne, akishinda  miwili na kutoka sare moja na kupanda kutoka nfasi ya tisa hadi ya pili katika msimamo. Yanga iliifunga Prisons bao 1-0 na ikashinda idadi kama hiyo dhidi ya Biashara United na kutoka sare ya bao 1-1 na KMC na ilitoka 0-0 na Mbeya City. 

Kwa upande wa Vandenbroeck aliiongoza Simba kushinda michezo mitatu, iliifunga Lipuli mabao 4-0, ikaifunga KMC mabao 2-0 na pia ikaifunga Ndanda mabao 2-0 na kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi, huku Mgunda akiiongoza Coastal kushinda michezo miwili, iliifunga Azam FC bao 1-0, kisha ikaifunga Mbeya City mabao 2-0 na kupanda kutoka nafasi ya sita hadi ya tano.

No comments:

Post a Comment

Pages