January 03, 2020

Naibu Waziri aridhishwa na miundombinu Shule ya Sunni Muslim Jamaat

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (katikati), akioneshwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sunni Muslim Jamaat, Salim Turky, sehemu ya majengo alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya shule hiyo jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu).
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sunni Muslim Jamaat, Salim Turky ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Mpendae Zanzibar akizungumza wakati Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya shule hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (katikati), akifafanua jambo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (kulia), akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sunni Muslim Jamaat, Salim Turky, ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mpendae Zanzibar alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya shule hiyo jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha (wa tatu kushoto), akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sunni Muslim Jamaat, Salim Turky ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Mpendae Zanzibar alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya shule hiyo jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, ameridhishwa na miundombinu ya Shule ya Sunni Muslim Jamaat (SMJ) ya Dar es Salaam na kwamba licha ya kukosekana kwa uwanja wa michezo, inapaswa kutazamwa kwa jicho la tatu kuiwezesha kusajiliwa kutoa huduma.

Naibu Waziri Ole Nasha alifanya ziara ya ukaguzi huo kwa niaba ya Waziri Joyce Ndalichako, akakiri kuwa SMJ iko katika mazingira mazuri, yaliyozungukwa na miundombinu bora, lakini inabanwa na Sheria ya Ukubwa wa Eneo la ujenzi wa shule kuwa hekari tatu, ambayo inapaswa kufanyiwa tathmini.

“Huduma zote muhimu zipo hapa, kasoro uwanja tu, na hapa ni mjini, kupata eneo la kutosha kujenga uwanja ni ngumu. Kama wizara tutajadili - kwamba ikitokea shule ikiwa na huduma zote bora na muhimu, lakini kasoro uwanja tu, tunafanyaje?” alisema Ole Nasha.

Aliongeza kuwa, Sheria inataka ukubwa wa eneo la shule inayopaswa kupewa usajili wa kudumu kuwa na hekari tatu, lakini wanapaswa kuziweka sheria hizo kwa kuzingatia mazingira yaliyopo, hususani kwa wawekezaji wanaojenga shule mijini.

“Mazingira ya miji mikubwa kama Dar, ukizingatia kila shule iwe na uwanja, kuna zitakazofungwa, kwa sababu nyingi hazina viwanja, kutokana na ufinyu wa maeneo. Kama wizara tumeanza kuona changamoto katika kulazimisha baadhi ya sheria.

“Kwa mfano; sheria inataka kusajili Shule ya Msingi - iwe na madara sita, ofisi ya walimu, nyumba mbili za walimu na vyoo vya kutosha, sasa swali linakuja, inapotokea wananchi wamejitahidi kujenga shule ya madarasa matano, unawezaje kuwanyima usajili kisa hawana darasa moja?

Alisema katika vikao vijavyo, watajaribu kuzifanyia tathmini sheria hizo, ili kutoa fursa pana kwa wadau wa elimu kuanzisha na kusajili shule zao, ambazo zinapoanza hutumika darasa moja na sio yote kwa mpigo, hivyo watakapofikia kujaza nadarasa yote, shule inaweza kuwa imejiongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sunni Muslim Jamaat, Salim Hassan Turky, ambaye pia ni Mbunge wa Mpendae visiwani Zanzibar, alimshukuru Waziri Ndalichako kwa kukubali kutembelea shule hiyo, lakini kutokana na msongo wa majukumu, akamtuma Naibu Waziri Ole Nasha.

“Tumefarijika sana sisi Sunni Muslim Jamaat kwa kututembelea kuona utendaji wetu. Tumekuwa tukiwaita wizara kuona shule na miundombinu yetu, kwa ujio huu sasa, Naibu Waziri utaona namna tulivyo ‘serious’ katika hili.

“Sheria ya ujenzi wa shule katika eneo la heka tatu inatubana, kwani tumefanya hivyo katika eneo la ukubwa wa heka moja na nusu. Hatuna uwanja wa michezo, lakini kila wiki watoto wanashiriki michezo kwa kulipia uwanja pale JMK Youth Park,” alisema Turky maarufu kwa jina la White.

Alishukuru kilio cha SMJ kusikika wizarani na kwamba wanaamini Naibu Waziri akitoka shule hapo, vikao vitakavyofanyika wizarani vitatumia busara katika kuridhia ombi la usajili na kukidhi kiu ya wanafunzi walionao shuleni hapo kupata elimu.

Aidha, Turky alisema wanaamini ombi la usajili wa shule yao litafanikiwa, lakini ikitokea wakakataliwa, wataheshimu maamuzi ya wizara na kuwa watawapeleka wanafunzi wazo (175 wanaosoma shuleni hapo hadi sasa) katika shule zinazokidhi mahitaji ya kisheria.

No comments:

Post a Comment

Pages