January 01, 2020

RT KUMPELEKA GULAM JAPAN

Picha tofauti zikimuonyesha mwanariadha mahiri wa mbio fupi kutoka Zanzibar, Ally Gulam, akimshukuru Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, baada ya kupewa fursa ya kusaka kufuzu Olimpiki ambapo atapiga kambi nchini Japan yatakapofanyika mashindano hayo.
 

Na Mwandishi Wetu
 
SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limepanga kumpeleka kambini mwanariadha, Ally Gulam, nchini Japan hivi karibuni, kwa lengo la kujiandaa na michuano ya Olimpiki itakayofanyika Julai, mwaka huu.

Michuano ya Olimpiki mwaka huu inatarajia kuanza Julai 24 hadi Agosti 9, itakayo fanyika jijini Tokyo, nchini Japan kwa kushirikisha michezo mbalimbali kutoka kwa wawakilishi wa mataifa tofauti ikiwemo Tanzania.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa RT, Tullo Chambo, alisema wamepanga kuongeza idadi ya wanariadha katika mashindano hayo mwaka huu  kwa mbio ndefu na za kati.

Hadi sasa wanariadha ambao wanauhakika wa kushiriki michuano hiyo ya Olimpiki, ni Alphonce Simbu pamoja na Failuna Matanga, ambao nao wataingia kambini kujiandaa hivi karibuni.

“Mwanariadha mahiri Ally Gulam, tumemuandalia kambi nchini Japan na hivi karibuni ataelekea huko, lengo ni kuangalia namna gani Tanzania itavuna idadi kubwa ya medali kulinganisha na miaka iliyopita,” alisema Chambo.

Alisema joto la mashindano hayo linaendelea kupanda na viongozi wa RT wanaendelea na mikakati ya kuwaandaa wafukuza upepo wao na kuwaweka kambi tayari kwa vita hiyo inayosubiriwa kwa hamu.

Chambo, alisema jumla ya wanariadha wawili pekee ndio wamefuzu kushiriki Olimpiki mwaka huu na waliobaki wanaendelea kusaka muda utakao wapa tiketi ya kushiriki mashindano hayo.

“Maandalizi yanakwenda vema, kama ambavyo tulisema awali wale ambao walishafuzu nao ni Simbu (Alphonce), pamoja na Failuna Matanga wataingia kambini nchini Kenya na ambao bado tunaendelea na mipango mikakati kujua namna gani watakata tiketi ili wajumuike na wenzao katika maandalizi ya kwenda kuipepoerusha vema bendera ya Tanzania,” alisems Chambo.

No comments:

Post a Comment

Pages