January 09, 2020

Wakufunzi 474 wapata mafunzo ya TEHAMA

Na Irene Mark

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa Wakufunzi 474 wa walimu tarajali jijini Dar es Salaam na Dodoma.

Mafunzo hayo yamehusisha wakufunzi zaidi ya 1,300 kutoka vyuo vyote 35 vya ualimu hapa nchini kwa ufadhili wa Serikali ya Canada na Wizara ya Elimu Chini ya Mradi wa Teachers Eduacation Support Programe (TESP), uliogharimu Sh. Bilioni 1.037.

 Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu anayesimamia Taasisi zote za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sebastian Inoshi, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha sekta ya elimu inaboreshwa kuanzia kwenye miundombinu, vifaa na uwezo kwa wakufunzi.

“Tumeandaa mafunzo ya wakufunzi ili wawe na uweledi na maarafi ya kisasa hasa kwenye TEHAMA ili kuleta ufanisi na ubora wa walimu watakaowafundisha wanafunzi wa shule za sekondari na msingi… lengo ni kutoa mazao bora ili kuharakisha maendeleo, haya ni mafunzo ya siku 10 yakijumuisha wakufunzi 205 kwa hapa Dar es Salaam na wengine 269 waliopo Dodoma, nia njema ya serikali ni kutaka elimu bora kwa taifa hili,” alisema Inoshi.

Mratibu wa mafunzo hayo, Menard Sikana kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, aliishukuru wizara hiyo na ubalozi wa Canada kwa kunuia kuiboresha sekta ya elimu hapa nchini na kupitia mradi wa TESP.

“Mafunzo haya ni muendelezo wa shughuli za mradi huu wa miaka mitano kuanzia 2017/2018 hadi 2022/2023 ambao ni kuboresha miundombinu ya vyuo vyote 35 vya ualimu ikiwemo kujenga upya Chuo cha Ualimu Kabanga, kuweka vifaakazi na sasa kuwekeza kwa wakufunzi wenyewe katika elimu ya TEHAMA.

“Mradi umejikita kwenye manunuzi ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia zikiwemo kopyuta, projekta na kuunganisha kwenye mifumo ya interneti hadi kwenye mkongo wa taifa ambapo vyuo vyote 35 vya ualimu vitaunganishwa.

“…Awali tulitoa mafunzo kwa somo husika yaani ‘content’ kwa wakufunzi wote karibu 1,300 baada ya kumaliza hatua hiyo sasa tunawawezesha kwenye matumizi ya Tehama kwa kujifunza na kufundishia, tulianza Agosti mwaka jana,” alisema Sikana.

Mratibu huyo alisema vyuo hivyo vimegawanywa kwenye kanda saba ambazo ni Kanda za Kaskazini, Kati, Ziwa, Magharibi, Nyanda za Juu Kusini, Kusini na Mashariki huku akibainisha kwamba washiriki wa Dar es Salaam walitoka kwenye vyuo vya Patandi, Monduli, Marangu, Mandaka, Korogwe Singachini na Mamile.

Baadhi ya wakufunzi waliozungumzia mafunzo hayo waliipongeza wizara kwa kudhamiria kuboresha elimu huku wakishauri mafunzo hayo kuwa endelevu ili kwenda sawa na mabadiliko ya teknolojia.

Wakuru Manini mkufunzi kutoka Chuo cha Ualimu Patandi, alisema ni mafunzo muhimu katika kuendeleza ubora wa elimu ili kukabiliana na changaomoto za ufundishaji huku akiamini kwamba wanafunzi watakaotoka kwenye mikono yao watakuwa walimu bora kwa shule za msingi na sekondari watakazokwenda kufundisha.
Sebastian Inoshi, Mkurugenzi Msaidizi Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, akizungumza na Wanahabari baada ya kuhitimisha siku 10 za mafunzo ya TEHAMA kwa Wakufunzi 205.
Mratibu wa mafunzo ya Wakufunzi kuhusu TEHAMA, Menard Sikana.
 Baadhi ya wakufunzi waliopata Elimu ya TEHAMA wakiwa darasani.

No comments:

Post a Comment

Pages