April 24, 2020

Makondakta wahimizwa kutembea na ‘Sanitaiza’

Kondakta Noah Jeremia wa daladala inayofanya safari za Tandika Makumbusho jijini Dar es Salaam, akiwaminyia kitakasa mikono 'Sanitaiza' abiria walipanda daladala anayofanya kazi ikiwa ni moja ya jitihada za kupambana na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19,anachofanywa kondakta huyu kinapaswa kuigwa nahudumu wa vyombo vya usafiri vya umma wote ili kukabiliana na janga hili. (Picha na Suleiman Msuya).



Na Suleiman Msuya

WAHUDUMU wa vyombo vya usafiri wa umma (Kondakta) wameshauri kutembea na vitakasa mikono ‘Sanitaiza’ kwenye magari yao ili kutumia wao na abiria kama moja ya njia ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.

Ushauri huo umetolewa na Kondakta Noah Jeremia, anayefanya kazi kwenye daladala inayofanya safari kutoka Tandika wilayani Temeke hadi Makumbusho Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Jeremia alisema yeye na dereva wake wamelazimika kutembea na ‘Sanitaiza’ kwenye gari kama kinga kwani hawajui abiria wanaopakia wameambukizwa COVID-19 au la.

“Sisi tunapakia abiria wa aina tofauti hatuna kipima joto hivyo njia sahihi ambayo tunaweza kujikinga ni kutumia maji na ‘Sanitaiza’ kwani hata wataalam wanaelekeza kufanya hivyo,” alisema.

Jeremia alisema amekuwa akiwapa ‘Sanitaiza’ abiria wake kabla ya kuchukua nauli ili kuhakikisha anakuwa salama na kuepuka maambukizi.

Kondakta huyo alitoa wito kwa wenzake kutembea na ‘Sanitaiza’ katika daladala zao na magari ya mikoani kwani inasaidia kupambana na gonjwa hilo hatari.

“Najisia faraja sana kwani abiria wanatoa ushirikiano unapowapa ‘Sanitaiza’ jambo ambalo linaonesha kuwa wananchi wameelewa changamoto hii ambayo inakumba dunia,” alisema.

Alisema iwapo jamii itaendelea kutoa ushirikiano ni dhahiri kuwa COVID-19 itaweza kudhibitiwa kwa haraka na jamii itaendelea na shughuli zake kwa uhuru.

Jeremia alisisitiza jamii kufuata maelekezo ya wataalam kuhusu mapambano dhidi ya COVID-19 ili kuhakikisha malengo yanafikiwa ya kutokomeza gonjwa hilo.
COVID-19 ni ugonjwa ambao umekumba Zaidi ya watu milioni 2.8 duniani kote ambapo Zaidi watu 180,000 wamefariki dunia huku Tanzania ikiwa na wagonjwa 284 hadi sasa, 48 wakipona na 10 wakifariki dunia.


No comments:

Post a Comment

Pages