May 11, 2020

KALIUA YAENDELEA KUPATA HATI SAFI MIAKA MITATU MFULULIZO

Mgambo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua akimpima joto jana  Mkuu wa Mkoa wa Ttabora Aggrey Mwanri (kushoto), kabla ya kuhutubia Baraza la Madiwani la kupitia taarifa   ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) za mwaka 2018/19. (Picha na Tiganya Vincent-Ofisi ya RC Tabora).
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akihutubia jana Madiwani wakati kikao cha kupiia taarifa za  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) za mwaka 2018/19.
Madiwani wakiwa  wa kikao cha Baraza la  Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua huku wakichukua tahadhari ya kujikinga kujikinga na virusi vya Corona.


 Na Tiganya Vincent
 
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua imepongezwa kwa kuendeleza kupata Hati inayoridhisha kwa miaka mitatu mfulululizo ya fedha.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Kaliua cha kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).

Alisema wamepata hati hiyo baada ya taarifa za fedha kuwa zimemridhisha Mkaguzi kuwa zimezingatia viwango vya uandaaji wa hesabu unaokubalika na hazina makosa makubwa.

Mwanri alisema tangu mwaka wa fedha wa 2016/17 hadi mwaka 2018/19, Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua imepata Hati safi jambo limeonyesha kuwa kuna usimamizi mzuri wa rasilimali mbalimbali.

Aliitaka Menejimenti kushirikiana na Baraza la Madiwani kuhakikisha kuwa wanaendelea na usimamizi mzuri wa rasilimali zao ili wasije kuchafua heshima waliyopata kwa kipindi cha miaka mitatu ya fedha.

“Tunawapongeza kwa kupata hati safi…lakini kupata hati safi sio kwamba mna mfumo wa udhibiti wa ndani wenye ufanisi wa asilimia 100 …inamaanisha kuwa hakuna jambo lolote kubwa lililobainika na Mkaguzi kumfanya atoe hati yenye shaka…angalieni isiye ikawa kama methali inayosema mgema akisifiwa tembo hulitia maji” alisisitiza.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alilipongeza Baraza la Madiwani kwa kuisimamia vizuri Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua na kuweza kufanya vizuri katika usimamizi wa rasilimali zake.

No comments:

Post a Comment

Pages