May 02, 2020

MAWAKALA WA MABASI KUPEWA VITAMBULISHO KUZUIA MSONGAMANO

Wamiliki wa vyombo vya Usafiri mkoani Tabora wakiwa katika kikao cha kujadiliana na uongozi wa Ofisi ya mkuu wa mkoa na Jeshi la Polisi namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid -19 wakati wa uendeshaji wa shughuli zao za kila siku. (Picha na Tiganya Vincent).
 
 
Na Tiganya Vincent
 
 
WAMILIKI wa Mabasi Mkoani Tabora wametakiwa kupeleka orodha ya mawakala wanaowatumia katika shughuli zao ili wanaohitajika waweze kupewa vitambulisho ili kupunguza msongamano wa wapiga debe wasiohitajika kwa ajili ya kuwakinga watumiaji wa Stendi hiyo na  virusi vinavyosababisha  ugonjwa wa Covid -19.
 
Azimio hilo limefikiwa jana mjini Tabora wakati wa kikao kati ya uongozi wa Mkoa wa Tabora na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji wa abiria.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora atapokea majina kutoka kwa wamiliki wa mabasi na kuandaa vitambulisho maalumu ambavyo ndio vitawaruhusu kuingia katika stendi mbalimbali kwa ajili ya kukatisha tiketi na shughuli nyingine za kuwahudumia wateja.

Alisema baada ya vitambulisho hivyo watu ambao watakutwa hawana vitambulisho na sio wasafiri watakamatwa na kushitakiwa kwa kusababisha fujo na kuhatarisha maisha ya wasafiri.

Awali Kamanda wa Polisi wa Usalama barabarani (RTO) Mkoa wa Tabora Gabriel Chiguma alisema waliendesha zoezi la kuwatambua watu wanafanyakazi katika Stendi ya Tabora na kubaini kuwa kuna wapiga debe 400 na Mawakala 400 jambo linalosababisha msongamo mkubwa katika Stendi ya Manispaa ya Tabora.

Alisema idadi hiyo ilikuwa kubwa sana na kutokana na janga la ugonjwa covid -19 walikubaliana na wamiliki wa mabasi wawapunguze ili kuondoa msongamano katika Stendi hiyo.

Chiguma alisema baada ya makubaliano na wamiliki wa mabasi kuwa wabaki mtu mmoja awe ofisi na mwingine Stendi wameshaanza kuwakata ambao hawakupendekezwa na wamiliki wa magari.

 Naye Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri wa Ardhini (Latra) Mkoa wa Tabora Nelson Mmari alisema stendi ya Tabora ina Mawakala wengi ukilinganisha na Stendi za maeneo mengine hapa nchini.

Alisema hatua hiyo inasababisha kero kwa wasafiri na wakati mwingine kuwatoza nauli iliyo nje ya utaratibu na wakati mwingine kusabiabishs upotevu wa mizigo ya abiria.

Mmari alitoa mfano wa nauli halali kutoka Sikonge hadi Tabora , ni shilingi 3,100/- lakini Wapiga Debe na Mawakala wanatoza shilingi 4,000/- na kuongeza kuwa kutoka Tabora kwenda Dar es salaam, abiria akilipa shilingi 40,000/- ,mpiga debe analipwa shilingi 5,000/=.

Alisema wamiliki wa Mabasi wanaweza kupata faida bila kuwa na msongamano wa wapiga debe.
Mmari alisema ni jukumu la Wamiliki wa Stendi za Mabasi kuroodhesha watu wanaowatumia kama Mawakala na Manispaa ya Tabora kama mmiliki wa Stendi kutengeza Vitambulisho ambavyo vitawatofautisha na wasio Mawakala ili wachukuliwe hatua kuondoa msongamano.

No comments:

Post a Comment

Pages