May 10, 2020

WAKUSANYAJI MAPATO MKOANI TABORA AMBAO HAWAJAPELEKA FEDHA BENKI KUCHUKULIWA HATUA

Na Tiganya Vincent

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeagiza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa watumishi wote waliopewa mashine za kukusanyia mapao (POS) ambao hadi hivi wadaiwa mapato waliyokusanya kwa kutoyawasilisha Benki.

Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Mkoa wa Tabora Msalika Makungu wakati wa kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Urambo.

Alisema kitendo hicho ni kinyume cha kifungu cha 60 cha Sheria ya fedha za umma yam waka 2001.
Makungu alisema dosari za aina hiyo ndio zimekuwa zikisababisha upotevu wa fedha za umma na kuziagiza Halmashauri kuhakikisha zinasimamia kwa ajili ya kuziondoa.

Aidha Katibu Tawala huyo wa Mkoa amepiga marufuku kwa Wakurugenzi na Waweka Hazina kuruhusu utaratibu wa Wakusanyaji mapato kuchukua asilimia zao(commission) kutoka makusanyo ya fedha za mapato ya ndani kabla ya kupelekwa Benki.

Alisema vitendo hivyo vinasababisha matumizi ya pesa  ‘mbichi’ na kupelekea Halmashauri kupoteza mapato yake na kusababisha uzalishaji wa hoja za kiukaguzi.

Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Tabora ameziagiza Menejimenti za Halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha hazizalishi madeni yanayotokana na stahili za watumishi wanahama na wale wanaopandishwa madaraja.

Alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishaagiza hakuna mtumishi atayehamishwa bila kulipwa stahili na kuongeza kuwa kwenda kinyume cha hapo ni kutenda kosa.

Makungu aliongeza kuwa kuchelewa kulipa stahiki za watumishi kunavunja morali ya kufanyakazi jambo ambalo linaweza kusababisha mgawanyiko miongoni mwa Watumishi.

Aidha Katibu Tawala huyo aliagiza Halmashauri zote kuanza kuandaa stahiki za posho za Madiwani ili Mabaraza yatakapovunja wasipate usumbufu wa kufuatilia.
 Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo wakiwa jana katika kikao cha robo ya tatu huku wakiwa wamechukua tahadhari ya kujikinga na Virusi vya Corona.
 Katibu Mkoa wa Tabora Msalika Makungu akihutubia jana  kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Urambo.
Mkuu wa Wilaya ya Urambo Angelina Kwingwa akichangia hoja wakati wa  kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Urambo kilichofanyika jana.

No comments:

Post a Comment

Pages