May 09, 2020

WAZIRI KAMWELWE AZINDUA MFUMO WA TIKETI MTANDAO


 Na Mwandishi Wetu 

WAZIRI wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (pichani) amezindua  mfumo wa majaribio wa ukatishaji tiketi  wa mabasi  kwanjia ya mtandao huku akieleza kuwa  njia hiyo italeta tija kwa serikali,abiria,na wamiliki wa mabasi.

Akizungumza  jana mara  baada ya uzinduzi huo Mhandisi Kamwelwe alisema mfumo wa ukatishaji tiketi kwanjia ya mtandao utaondoa upotevu wa mapato kwa wasafirishaji ambayo mara nyingi hupotelea katika mikono ya wapiga debe.

"Utawawezesha wasafirishaji kukopesheka kwa urahisi kwani taarifa za miamala yao zitaakisi moja kwa moja katika mabenki,pia utasaidia kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta kutokana na kuongezeka kwa mapato"alisema .

Mhandisi Kamwelwe alisema kwa upande wa abiria matumizi ya mtandao katika ukatishaji tiketi utawaondolea abiria mlolongo wa kufunga safari kwenda vituo vya mabasi siku moja kabla ya safari waajili ya kukata tiketi.

"Pia utaondoa kero za abiria kubughudhiwa kwenye vituo vya mabasi na kufanya usafiri huu kuwa na heshima,utakomesha vitendo vya upandaji holela wa nauli hasa kipindi cha mwisho wa mwaka "alisema.

Alisema kwa upande wa serikali mfumo huo utawezesha kupatikani kwa taarifa muhimu zenye kusaidia serikali kufikia maamuzi sahihi kwakuwa ndio kitovu cha usafirishaji nchini.

"Mfumo huu utaisaidia Mamlaka ya Usafiri Ardhini (LATRA) kutambua idadi ya watu wanaosafiri kwenda maeneo mbali mbali hivyo LATRA itapanga huduma za usafiri kulingana na mahitaji ya eneo ya njia husika,mamlaka zinazohusika zitakuwa na uwezo wa kupanga sera za usafirishaji na ujenzi wa miundombinu kutambua maeneo ya kipaumbele ya usafirishaji"alisema .

Mhandisi kamwelwe alisema mfumo huo utatumika kwa majaribio hadi kufikia juni mwaka huu na baada ya hapo LATRA isitoe leseni kwa mmiliki ambaye hajajiunga na mfumo huu ili kuhakikisha kila mmiliki a natumia mfumo huu.

"Kufikia Septemba mwaka huu utekelezaji uanze kwa upande wa dalala nawaagiza kusimamia kanuni kikamilifu hususan mfumo huu kila atakaye kuja kuchukua leseni lazima aunganishwe na mfumo huu"alisema

Kwa upande wake Mkurugenzi LATRA Gilliad Ngewe alisema kupitia mfumo huo watoa huduma hawatodanganywa tena kuhusu mapato yao kwani kila abiria anapokatishwa tiketi moja kwa moja hela ya mmiliki itakwenda benki na mwenyewe kupatiwa ujumbe kiasi cha pesa na idadi ya wateja watakao hudumiwa kwa siku .

"Tajiri atafunga mahesabu mwenyewe na si wakala tena ,tumejipanga kikamilifu kusimamia utoaji huduma kwa mfumo huu na maafisa wetu watashirikiana na jeshi la polisi kutoa elimu kuhakikisha wananchi wote wananufaika na mfumo huu na tutakuwa na kituo cha huduma kwa wateja ambacho kitazinduliwa hivi karibuni watu kupitia namba 0800110150 watapiga na kupata elimu juu ya mfumo huu"alisema.

Alisema mwananchi kwa kutumia simu ya mkononi ataweza kununua tiketi ya basi analotaka aina ya kiti na kupangiwa muda wa safari.

Alisema katika ulipaji wa tiketi abiria ataletewa ujumbe kwenye simu ujumbe ambao utampa maelekezo ya kufanya malipo na mara baada ya kukamilisha atapatiwa ujumbe mwingine ambao utakuwa tiketi yake atakayolazimika kuitunza ili kuingia nayo katika basi.

Pia kwa abiria ambao hawatakuwa na simu janja hawatosumbuka Kwani watakapofika vituoni watakatiwa tiketi hizo kwa kifaa maalumu POS .

Mbali na hilo alisema abiria watanufaika zaidi Kwani  kwa kutumia mfumo huo  watakuwa na uwezo wa kuchagua kituo cha kupanda basi pamoja na kushuka.

Mkurugenzi wa Imani Class Amani Kaganda ambaye tayari ameanza kutumia mfumo huo kwa majaribio alisema faida za mfumo huo ni mkubwa kwani mmiliki wa basi anajua fedha alizoingiza kwa siku na kuanza kupanga matumizi yake .

"Fedha naipata kwa wakati sisumbuki na watu kunipa hesabu pia nina uhakika na abiria wanaoingia kwenye gari"alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages