July 16, 2020

BINTI WA NDESAMBURO ACHAGULIWA KUGOMBEA UBUNGE MOSHI VIJIJINI

Lucy Owenya mtoto wa Mbunge wa zamani wa jimbo la Moshi mjini Philemoni Ndesamburo akizungumza wakati akiomba kura katika uchaguzi wa kura za maoni za kumpata atakayegombea Ubunge katika jimbo la Moshi vijijini kupitia Chadema.
Wakili Sisty Massawe ni miongoni mwa waliojitokeza kuwania nafasi ya kugombea Ubunge katika jimbo la Moshi vijijini akizungumza na wapiga kura.
Wagombea wa nafasi ya Ubunge jimbo la Moshi vijijini kupitia Chama cha Demokrasia (Chadema) wakisubiria matokeo wakati wa uchaguzi uliofanyika katika eneo la Garden ,kutoka kulia ni Lucy Ndesamburo ,Sisty Massawe na Emanuel Nyaki.


Na Dixon Busagaga, Moshi 

MTOTO wa Mbunge wa zamani wa Jimbo la Moshi mjini Philemoni Ndesamburo ,Lucy Ndesamburo ameshinda katika kura za maoni za kuwania kuteuliwa na Chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) kugombea Ubunge  katika Jimbo la Moshi vijijini.

Hii ni mara ya pili kwa Lucy Ndesamburo kushinda katika kura za maoni katika jimbo hilo ambapo mwaka 2015 alimshinda mpinzani wake Anthony Komu kwa zaidi ya kura 300 .

Katika kura hizo za maoni, Lucy  ameibuka na ushindi wa kura 129  sawa na asilimia 94. 2 huku wapinzani wake  Emanuel Nyaki akipata kura 04 sawa na asilimia 2.9 na Sisty Massawe akipata kura 4 sawa na 2.9.

Akitangaza matokeo ya kura hizo za maoni, msimamizi wa uchaguzi, Ephata Nanyaro, amesema wajumbe waliopiga kura ni 137 na kwamba mchakato unaoendelea kwa sasa ni wa kamati kuu ya chama


Akizungumza Lucy, baada ya matokeo hayo, mbali ya kushukuru, amewataka wajumbe kushirikiana ili kuhakikisha chama kinashinda katika ubunge na hata nafasi za udiwani


Naye Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila, amewataka wanachama wa chama hicho kuwa wamoja na kushikamana ili kuweza kukipatia chama hicho ushindi.

Katika uchaguzi wa kura za maoni uliofanyika mwaka 2015 Lucy  aliyekuwa mwanamke pekee katika kinyang’anyiro hicho kati ya wagombea tisa, aliibuka mshindi kwa kupata kura 266 dhidi ya 25 alizopata Antony Komu.

Hata hivyo, baada ya kushinda, kamati kuu haikurudisha jina lake na badala yake ilirudisha jina la Komu ambaye sasa amehamia NCCR- Mageuzi

No comments:

Post a Comment

Pages